LEO na kesho timu zetu zitakuwa viwanjanii katika mashindano ya ngazi ya klabu yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Yanga yenyewe itashuka Uwanja wa Taifa Dar es Salaam kuikabili Al Ahly ya Misri katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati kesho Azam itakuwa Chamazi kuikabili Esperance ya Tunisia katika Kombe la Shirikisho.
Yanga imeingia raundi ya pili ya michuano hiyo na kwa sasa inashikilia uwakilishi kwa Tanzania na Afrika Mashariki baada ya klabu nyingine za ukanda huo zilizokuwa zikishiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kutolewa.
Watanzania wote tuna imani kwamba timu zetu zitashinda, maana ndio njia ya kusonga mbele, vinginevyo hadithi itakuwa imeishia hapo. Kutokana na hali hiyo, tunawaombea heri Yanga na Azam kwamba Watanzania tupo nyuma yao, hakuna lisilowezekana panapokuwa na juhudi za kutosha.
Tunaamini Yanga na Azam watatumia vyema viwanja vya nyumbani na watawapa mashabiki furaha na si karaha, kwani ndoto yao ni kufikia mafanikio makubwa zaidi. Ni vyema mashabiki wote bila kuangalia klabu gani wanayoipenda hapa nchini, washirikiane kuzitakia heri timu zote na bila shaka dua zao zitafika mahali husika.
Tuna kila sababu ya kuona michezo yao ina umuhimu mkubwa kwetu sisi Watanzania hasa kipindi hiki tunachohaha kujaribu kuinua soka letu. Kwa upande wa wachezaji wenyewe nao lazima wahakikishe wanapigana kufa au kupona ili ushindi upatikane.
Tunaamini wachezaji wa timu zote wamejiandaa vya kutosha, wamepewa kila aina ya hamasa na pia wamelipwa vizuri ili wasiwe na malalamiko badala yake wawe na kazi moja tu ya kuhakikisha wanaleta ushindi.
Lakini kikubwa tunawasihi Watanzania tuweke kando tofauti zetu za klabu, badala yake tushirikiane kuhakikisha timu zetu zinavuka hatua hii na kwenda mbele zaidi. Wenzetu nchi nyingine linapokuja suala la kimataifa wanakuwa na ushirikiano, tukumbuke timu zetu zikifanikiwa zitakuwa zimeitangaza nchi, wala si kitu kingine na nchi ikitangazwa ni jambo zuri kwetu sote.
Hata hivyo, wachezaji watambue hakuna njia ya mkato wala hawawezi kufika mbali kwa kuandikwa vizuri magazetini ama kuombewa dua, bali wapambane uwanjani.
Wanacheza na timu za Afrika Kaskazini, tuna sababu ya kushinda mechi za nyumbani ili tujiweke pazuri kwa mechi za ugenini. Si kushinda tu bali kuhakikisha tunapata ushindi mnono na wa kishindo ili hakika tuweze kujiwekea mazingira mazuri mechi za marudiano na iwe rahisi hata kwenda kulilia sare tu.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment