Image
Image

Kutumbuliwa kwa KILANGO kuwe funzo kwa mliobaki.


HABARI iliyopata nafasi kubwa kwenye vyombo vya habari mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii juzi na jana, ni uamuzi wa Rais John Magufuli kutengua nafasi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela.
Kilango ametumikia nafasi hiyo kwa muda mfupi tu, usiozidi mwezi mmoja na kuondolewa kwake kumetokana na kutoa taarifa zisizo sahihi za kuonesha mkoa wake wa Shinyanga, hauna mfanyakazi hewa hata mmoja.
Lakini, Rais Magufuli, kwa maneno yake, alisema aliunda timu ya maalumu hivi karibuni kuhakiki watumishi hao na tayari timu hiyo imebaini kuwepo kwa watumishi hewa 45 mkoani Shinyanga.
Watumishi hao hewa walikuwa wameshalipwa mishahara ya jumla ya Sh milioni 333.9. Fedha hizo ni za mishahara ya mwezi mmoja tu. Rais anasema bado wilaya mbili za mkoa huo za Ushetu na Shinyanga Vijijni, hazijafikiwa na timu hiyo ya uhakiki.
Sisi tunaona kuwa uamuzi huo wa Rais Magufuli, kutengua uteuzi wa Kilango ni funzo kwa watumishi wote waliopo serikalini. Wanaopewa dhamana yoyote ya kazi, wazingatie weledi wa kazi yao, wajenge uaminifu kwa wajiri wao, wafuatilie kila kitu kwa walio chini yao na kufanya kazi kwa kuzingatia muda.
Kilango amewahi kupewa nyadhifa mbalimbali, kama vile mbunge na naibu waziri na kote huko alionesha kuwa kiongozi mchapakazi, mfuatiliaji na mwajibikaji. Lakini, akiwa huko Shinyanga, Kilango alishindwa kufanya kazi yake inavyostahili na aliwaamini walio chini yake, aliokutana nao kwa kipindi kifupi.
Ameshindwa kutambua siku zote kwenye dhamana yoyote, unayopatiwa hutakiwi kumwamini yeyote unayefanya naye kazi, kwani mara nyingi uzoefu unaonesha wabadhirifu ni walewale wanaokupatia taarifa. Hao ndiyo wanaoweza kukuangusha kwenye vita yoyote ya ubadhirifu.
Kilango pia ameshindwa kujipa muda kujiridhisha na taarifa aliyopewa na akakurupuka kuwasilisha taarifa hiyo wakati rais mwenyewe na wananchi wengi waliweza kujiuliza inakuwaje mkoa mkubwa kama Shinyanga, usiwe na watumishi hewa wakati hilo ni tatizo kwa nchi nzima.
Hilo limeshatokea na wengi wetu kama bado tulikuwa hatumfahamu Rais Magufuli, sasa tumtambue vizuri nini anataka kwenye kipindi chake cha uongozi; malengo yake ni kuipeleka nchi hii ngazi gani. Tuonavyo sisi viongozi waliobaki kwenye Serikali ya Rais Magufuli, wanatakiwa kumfahamu aina ya kiongozi wao aliyewapa dhamana hiyo.
Wanatakiwa kufuatilia kauli zake na matendo yake tangu akiwa waziri, wakati wa kampeni na hata baada ya kuwa rais. Mara kwa mara hasa wakati wa kampeni amekuwa akisema hana mzaha wala mchezo na mtumishi yeyote, atakayeharibu kazi na atamchukulia hatua hapohapo alipo na watu wasitegemee watakimbia mkoa kwa uhamisho.
Waswahili wanasema, ‘Ukiona mwenzio ananyolewa, tia maji’. Hivyo hilo lililomkumba Kilango, wakati wowote linaweza kumkuta mtumishi yeyote wa umma au kiongozi aliyeteuliwa na rais. Kama mtumishi unajiona huwezi kwenda na kasi, anayotaka Rais Magufuli ni vema ujiondoe mapema ili yasikukute yale aliyosema Rais Magufuli mwenyewe kuwa anapofanya sherehe ya kuteuliwa, pia ajiandae kufanya sherehe pale atakapoondolewa.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment