Takribani watu 9,000 wamepoteza maisha yao, thuluthi
moja ikiwa ni raia kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa. Mazungumzo hayo awali
yalipangwa kuanza Jumatatu lakini yakacheleweshwa baada ya waasi wa Kishia
nchini Yemen wanaofahamika kama Wahouthi na washirika wao kususia kuhudhuria.
Kumekuwa na majaribio ya awali ya kuandaliwa
mazungumzo ya amani. Duru hii ya mazungumzo yanayofanyika Kuwait inalenga
kutafuta mbinu za kuutatua mzozo baina ya serikali ya Yemen inayotambuliwa na
jamii ya kimataifa, na ambayo inaungwa mkono na muungano wa jeshi linaloongozwa
na Saudi Arabia, na Wahouthi na washirika wao, ambao wanayajumuisha wanajeshi
watiifu kwa aliyekuwa Rais wa muda mrefu Ali Abdullah Saleh.
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Kuwait Sheikh Sabah
al-Khalid al-Sabah, katika hotuba ya ufunguzi aliwaomba Wayemen waachane na
vita na kuchagua amani. "Kwa niaba ya Kuwait, serikali yake na watu wake,
ni furaha yangu kuwakaribisha ndugu zetu Wayemen katika nchi yao ya pili,
Kuwait, kushiriki katika mazungumzo ya Yemen chini ya uangalizi wa Umoja wa Mataifa
ili kutafuta ufumbuzi wa mzozo. Kupunguza umwagaji damu na kupunguza mateso ya
kibinadamu ambayo wamepitia na wanaendelea kupitia"
Jumla ya wajumbe 14 kutoka kila upande wanaripotiwa
kushiriki katika mazungumzo hayo, ambayo yanasimamiwa na mjumbe maalumu wa
Umoja wa Mataifa, Ismail Ould Cheikh Ahmed. "Ninawakaribisha kuhudhuria
mikutano ya kufikia suluhisho la kisiasa na kuondokana na mzozo huu. Barabara
ya amani inaweza kuwa ngumu lakini tunaweza kuitembea. Kuna mitazamo tofauti
lakini tunaweza kuwa na mitazamo ya pamoja. Kuna mianya mingi lakini kwa kuwa
fikira ni nzuri tunaweza kufaulu."
Siku moja tu kabla ya kuanza mazungumzo hayo,
Wahouthi walionya kuwa wangefuta ushiriki wao ikiwa ukiukwaji wa mpango wa
kusitisha mapigano ulioanza kutzekelezwa Aprili 10 ungeendelea. Pande zote
mbili za mapigano zimeukiuka mpango huo tete.
Jeshi la muungano likiongozwa na Saudia na
kuzijumuisha nchi nyingi za Kiarabu – ikiwemo Kuwait, ambayo ni mwenyeji wa
mazungumzo hayo – limekuwa likiwalipua Wahouthi tangu mwishoni mwa Machi 2015
kujaribu kuwadhoofisha na kuukamata tena mji mkuu wa Sanaa, baada ya wao
kumlazimu kaimu Rais wa Yemen Abed Rabbo Mansour Hadi kukimbilia uhamishoni.
Tawi la al-Qaeda nchini Yemen liliikamata miji kadhaa pamoja na ukanda wa pwani
na kundi linalojiita Dola la Kiislamu – IS, likajiimarisha nchini humo kufuatia
vita vya wenywe kwa wenyewe.
Na wakati mazungumzo hayo yakianza Kuwait,
wanamgambo wa Houthi na serikali ya Yemen walibadilishana wafungwa katika mji
mkuu Sanaa. Jumla ya wanamgambo 71 wa Kihouthi na wanajeshi 50 wa serikali
waliachiliwa huru.
0 comments:
Post a Comment