MKUTANO wa tatu wa Bunge la 11, umeanza leo mjini
Dodoma pamoja na mambo mengine, ambapo utnajikita kujadili na kupitisha Bajeti
ya Serikali ya mwaka 2016/17.
Ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Bunge Dar es Salaam
juzi,ilisema mjadala wa bajeti utaanza leo hadi Aprili 21.
“Baada ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa kujadiliwa,
Bunge litapokea na kujadili utekelezaji wa bajeti kwa wizara zote kwa mwaka wa
fedha 2015/16 na makadirio ya matumizi ya Serikali kwa mwaka 2016/17, kazi ambayo
itaanza Aprili 22 hadi Juni 2, mwaka huu,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo, ilisema Juni 9, waziri anayehusika na
mipango atawasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa nchi, ikifuatiwa na hotuba ya
bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17, kisha kufuatiwa na mjadala Juni
13 hadi 21.
“Ratiba inaonyesha kutakuwa na hati za kuwasilishwa
mezani, Bunge litapokea ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za
Serikali ya mwaka 2014/15 na majibu ya
Serikali kuhusu hoja zitakazotolewa na mkaguzi wa hesabu za serikali kwa mwaka
wa fedha 2014/15,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo, ilisema maswali 465 yataulizwa na
kujibiwa na Serikali bungeni, huku kila Alhamisi yataulizwa maswali kwa Waziri
Mkuu ambapo 88 yanatarajiwa kuulizwa na kujibiwa.
“Bunge pia linatarajia kujadili na kupitisha miswada
miwili ambayo ni muswada wa Sheria ya Matumizi wa mwaka 2016, kujadili na
kupitisha muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2016.
“Kutakuwa pia na uchaguzi wa mwenyekiti mmoja wa
Bunge ili kuziba nafasi iliyoachwa wazi, baada ya Spika kufanya mabadiliko ya
wajumbe wa baadhi ya kamati za kudumu za Bunge,” ilisema taarifa hiyo.
Katika mkutano huo, wabunge wapya wanne ambao ni
Mbunge wa Kijitoupele (Zanzibar), Shamsi Vuai Nahodha, Mbunge wa Viti Maalumu,
Ritha Kabati, Lucy Owenya na Oliver Semguruka wataapishwa.


0 comments:
Post a Comment