Kumekuwa na taarifa zinazoendelea kupotosha umma na
baadhi ya vyombo vya Habari kuwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC)
ilipokuwa ikitekeleza majukumu yake tarehe 5 Aprili, 2016 ililitaka Jeshi la
Polisi kuwasilisha Mkataba ulioingiwa Kati ya Jeshi hilo na Kampuni ya Lugumi
Enterprises Ltd kuhusu mradi wa Utambuzi wa Alama za Vidole AFIS (Automated
Fingerprint Identification System). Ofisi ya Bunge inapenda kutoa ufafanuzi
kuhusu jambo hili kwamba, taarifa hizo si za kweli na zina lengo la kupotosha
umma kutokana na kile kilicho amuliwa na kamati hiyo.
Ukweli kuhusu jambo hili ni kwamba tarehe 5 Aprili,
2016, kamati hiyo ilikutana na kujadili Taarifa ya Ukaguzi wa hesabu
zilizokaguliwa za fungu 28, Jeshi la Polisi kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni
30, 2014 ambapo kamati pamoja na mambo mengine ilibaini dosari katika
utekelezaji wa mkataba huo.
Kutokana na dosari hizo, kamati iliomba Afisa
Masuhuli ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mabo ya Ndani ya Nchi kuwasilisha
maelezo ya kina kwa maandishi kuhusu utekelezaji wa mradi huo kwa Ofisi ya
Katibu wa Bunge ili kamati iweze kuchambua na kujadili maelezo hayo kabla ya
kupendekeza kwa Bunge hatua zaidi za kuchukua. Kufuatia agizo hilo, kamati
ilimwandikia pia Katibu wa Bunge taarifa kuhusu agizo hilo tarehe 12 Aprili,
2016 ili kupatiwa maelezo hayo kutoka kwa Afisa Masuhuli.
Aidha, Ofisi ya Bunge ilimwandikia barua Katibu Mkuu, Wizara ya
Mambo ya Ndani tarehe 12 Aprili, 2016 kuwasiilsha Taarifa ya utekelezaji wa
maagizo ya Kamati Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyotokana na
kikao hicho cha tarehe 5 Aprili 2016 kabla ya tarehe 18 Aprili, 2018 kama
ilivyoshauriwa na kamati . Hivyo ni vyema Umma ukafahamu kuwa kilichoombwa na
Kamati ni Maelezo ya utekelezaji wa Mkataba huo na sio Mkataba kama
inavyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya Habari ambapo Ofisi ya Bunge iliomba
maelezo hayo yawasilishwe kabla ya tarehe 18 Aprili, 2016.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano Ofisi ya
Bunge DAR ES SALAAM
15 Aprili, 2016.


0 comments:
Post a Comment