Ni takribani miezi mitano tangu tumpate Rais mpya wa
Awamu ya Tano. Awamu ambayo inaongozwa na mtoto wa mfugaji tena msomi mbobevu wa Sayansi Dk. John Pombe
Joseph Magufuli.
Rais Magufuli ambaye kitaaluma ni Mwalimu mbali na
kubebwa na historia yake ya nyuma inayomchora kama kiongozi mfuatiliaji na
muwajibikaji, tangu apewe rungu la kuiongoza dola ameonekana kuwa kivutio
kikubwa kwa wananchi hasa wala mlo mmoja kwa siku.
Mtindo wake wa uongozi wenye kubeba vionjo vya
‘Tumbua majipi’ siyo tu umemfanya awe maarufu kwa muda mfupi ndani ya
Watanzania bali hata mataifa ya nje amekuwa gumzo vijiweni, maofisini, mitandao
ya kijamii na vyombo vya habari.
Ni vigumu kutambua siri inayombeba Magufuli
kuonekana anang’ara dakika za mwanzo wa mchezo japo dakika tisini si haba.
Inawezekana ni namna anavyopiga chenga kuelekea kwenye nyavu kwamba kwa muda
mrefu wananchi walikuwa wamemkosa mchezaji hodari ukizingatia waliyemtumainia
alishatangulia mbele ya haki.
Pamoja na uzuri wa Mheshimiwa Magufuli kucheza kwa
kasi ili apate bao la mapema ndani ya dakika tano za mwanzo, naanza kupatwa na
wasiwasi kwa namna mashabiki wake wanavyomshangilia huku wakipiga vuvuzela
badala ya kuangalia ni wapi mchezaji
huyu anaweza kujikwaa na kupata maumivu.
Nasikitika sana maana tangu Rais Magufuli aanze
kuongoza nchi pamekuwapo na kauli nyingi kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwamo
wananchi wa kawaida, viongozi wa dini, wasomi
na wanasiasa kwa ujumla wanaodai kuwa kiongozi huyu atiwe moyo ili asije
akakata tamaa.
Kwenye tamasha la Pasaka lililoandaliwa na Msama
Promotions na kufanyika Machi 27, mwaka
huu katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye alikuwa
mgeni rasmi katika tukio hilo
Nape Nnauye alisema Watanzania wamuunge mkono Rais katika harakati zake ili
asikate tamaa.
Wakati Nnauye akisema hayo, hata viongozi wengine kama Mwenyekiti wa
Wazazi wa CCM Taifa, Abdalah Bulembo na msemaji wa chama hicho, Sendeka kwa
nyakati tofauti wamekuwa wakisisitiza hivyo kwamba Rais asikatishwe tamaa.
Si hao tu waliosema hivyo bali hata shirikisho vyuo vya elimu ya juu Seneti
Mkoa wa Dar es Salaam liliwahi kutoa
tamko lake kwa kumuhakikishia, Dk. Magufuli kuwa watashughulika na
yeyote atakayejaribu kupanga kuihujumu au kuikwamisha Serikali katika
utekelezaji wa majukumu yake hususani ya kupambana na ukwepaji kodi, ubadhirifu
na usimamizi wa uwajibikaji kwa nguvu zote.
Hizo ni miongoni mwa kauli chache ambazo zimetolewa kwa siku za hivi karibuni
kama njia mojawapo ya kumuunga mkono Rais anayeonekana kuchukia machukizo
yanayowachukiza wachukizwaji.
Kimsingi kila binadamu hapa duniani mwenye damu na
nyama akifanya jambo jema hujihisi
vizuri akipewa motisho za vitu au nyama
ya ulimi ili aweze kusonga mbele na hii ndiyo asili ya maumbile yetu.
Lakini pamoja na binadamu kuhitaji kutiwa moyo
katika safari yake, kuna haja ya kuchukua tahadhari katika mazingira ambayo
yanaweza kusababisha mtu huyo asipate nafasi ya kukosolewa walau kidogo.
Wahenga waliosema, ‘Mgema akisifiwa tembo hulitia
maji’ hawakukosea maana
binadamu aliyezaliwa na mwanamke asipopata changamoto katika maisha mara nyingi hubweteka na
kujikuta akiboronga.
Sisemi kuwa ni vibaya kumpongeza Rais katika
harakati zake ukizingatia nchi yetu maji yalikuwa yamefika shingoni, lakini
itakuwa ni makosa makubwa kiongozi huyu kumchukulia kama Malaika Gabrieli
kwamba kila jambo analolifanya ni sahihi.
Ni
kutomtendea haki Rais kumchukulia kama yai lisilostahili kutikiswa ili
kuepuka lisipasuke, kumbe lingetikiswa kati ya mayai mengi ndipo tungegundua
ubora wake kama linafaa kwa matumizi.
Muigizaji, mtangazaji, mwanasiasa na Mwandishi wa
habari raia wa Uingereza, Mark Thomas aliwahi kusema, ukosoaji ni mrejesho wa
yale unayoyafanya ili kujua kama uko sahihi au la.
Kwa mantiki hiyo kama wananchi hawataki kuona Rais
akikosolewa ni hatari sana kwani kiongozi huyu anaweza kutumbukia kwenye shimo
ambalo watu wake walikuwa wanafahamu lakini wakanyamaza wakidhani kwa kufanya
hivyo ni kumlinda. Thomas anaendelea kusema kuwa ukosoaji ni mfumo wa
mawasiliano kwa maana ya kwamba wakosoaji hutaka kukupa mrejesho wa kile
unachokifanya kwao, ndiyo kusema ni fursa kwako kujifunza zaidi kuhusu watu
unaowafanyia kazi na kujua namna ya kuwapa utoshelevu.’’
Je, ni kwa namna gani Rais ataweza kujipambanua kama
yuko sahihi au la kama kila anayetaka kumkosoa ataoneka ni msaliti asiyemtakia
mema ? Ni kwa namna gani kiongozi huyu atapata nafasi ya kujifunza mambo mapya
kama kila jambo alifanyalo litaonekana ni mvinyo ?
Madhara ya kutomkosoa kiongozi ni makubwa kuliko
watu wanavyofikiria. Ikumbukwe Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete
kabla na wakati anaingia madarakani wananchi wengi walisahau kuwa ni binadamu na kubakia wanambatiza majina ya
utukufu badala ya kumkosoa kama njia ya kumsaidia.
Ben R. Mtobwa katika kitabu chake cha ‘Kikwete
safari ya Ikulu’ ukurasa wa 28 hadi 40
ameonyesha baadhi ya wananchi waliotoa mtazamo wao kuhusu ujio wa
Kikwete. Prince M. Bagenda ‘Kikwete ni
mtu mstaarabu,’ Kajubi Mukajanga: “Namfahamu JK kama mtu mcheshi, rahisi
kuingilika (accessible) na kuongea naye, mwenye tabasamu muda wote, lakini pia
mtu madhubuti anayejiamini.
Wengine ambao hawakuficha hisia zao ni Methodius
Kilaini sasa hivi Askofu Msaidizi Kanisa Katoliki Jimbo
la Bukoba, “Kikwete ni chaguo la Mungu, kwani maombi yetu ya muda mrefu
yamesikika” na Moses Kulola aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la EAGT sasa
Marehemu: “Tunamkubali Kikwete kama mtu wa watu na Mungu ametuchagulia, nipo
tayari hata kampeni”
Hakika binadamu ni popo, wazabizabina na wazandiki
maana wengi waliompongeza Rais Kikwete na kumuona kama mafuta ya senene huku
wakishindwa kumuonyesha njia sahihi hatimaye
wamekuwa wa kwanza kumlaumu makanisani, misikitini na kwenye vyombo vya
habari kwamba ameharibu nchi.
Kuna msemo usemao, ‘Ukubwa ni jaa’ hivyo Rais
Magufuli usiwachukie wanaokukosoa, kukubeza na hata kukutukana mwishowe ukaamua kuwaziba midomo kwa
kuwafungia magazeti, luninga na redio bali uwapende maana wanakusafishia njia.
Kumbuka wanaokusifia bila kukuonyesha
njia mwisho wa siku wanaweza kugeuka Yuda Iskariote.
0 comments:
Post a Comment