UONGOZI wa Simba umemsimamisha mechi tano beki wake,
Hassan Kessy kwa madai ya kuonesha utovu wa nidhamu katika mchezo wa Ligi Kuu
Tanzania Bara kati ya timu hiyo na Toto Africans kwenye Uwanja wa Taifa Dar es
Salaam, mwishoni mwa wiki iliyopita.
Adhabu hiyo inamaanisha Kessy atakosa mechi zote za
ligi zilizosalia za Simba ambazo ni dhidi ya Azam, Mtibwa, Majimaji, Mwadui na
JKT Ruvu.
Katika mechi hiyo ambayo Simba ilipoteza kwa bao
1-0, Kessy alimchezea faulo mshambuliaji Edward Christopher wa Toto na hivyo kutolewa
nje kwa kadi nyekundu.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam
jana, kocha wa Simba, Jackson Mayanja alisema uamuzi huo ulifikiwa kwenye kikao
cha viongozi wa Simba kilichokutana wiki hii.
“Ile rafu ilikuwa mbaya sana angeweza kumuua, kwa
hiyo uongozi umeona umsimamishe ili liwe fundisho kwa wengine wenye mtindo wa
kucheza rafu kama hizo ambazo mwisho zinaigharimu timu,” alisema.
Kuhusu madai ya kipa wa timu hiyo, Vincent Agban
kumpiga kofi Kessy, kocha Mayanja alisema hawajaliona suala hilo, lakini
wanalifanyia uchunguzi ikibainika watachukua hatua.
Tangu kutokea kwa tukio hilo, Kessy ambaye mkataba
wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu amekuwa akisakamwa na mashabiki,
wakimtuhumu kuchangia kipigo hicho. Tayari mchezaji huyo amekaririwa akisema
hataki kuongeza mkataba mwingine Simba.
“Kuanzia leo sitaenda mazoezini, maana nimechoka
kila siku kulaumiwa nahujumu,” alisema.
Wakati huo huo, Ofisa Habari wa timu hiyo, Haji
Manara alisema kikosi chote cha Simba kinatarajiwa kwenda Zanzibar leo kuweka
kambi ya maandalizi ya mechi zilizosalia. Simba inatarajiwa kucheza na Azam
kwenye Mei Mosi mechi inayotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Timu hiyo inashika nafasi ya pili kwenye msimamo
ikiwa na pointi 57 na Azam ni ya tatu ikiwa na pointi 55. Yanga ndio inaongoza
kwa kuwa na pointi 59.
0 comments:
Post a Comment