TIMU ya soka ya Simba jana ilipunguzwa kasi kwenye
mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu na kushindwa kurejea
kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo baada ya kuchapwa bao 1-0 dhidi ya Toto
Africans.
Kwa matokeo ya jana Simba ilishindwa kutamba katika
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kukosa pointi tatu muhimu ambao
zingewashusha kileleni watani wao wa jadi, Yanga wanaoongoza kwa pointi 59.
Wekundu hao wa Msimbazi wamebaki nafasi ya pili
kwenye msimamo wa ligi kwa kujisanyia pointi 57 baada ya kucheza michezo 25,
wakifuatiwa na Azam FC nafasi ya tatu kutokana na pointi 55 walizonazo baada ya
kushuka dimbani mara 24.
Simba waliingia uwanjani wakiwa na shauku ya kupata
bao la mapema ili waweze kukamata usukani, lakini mipango yao ilianza
kutibuliwa baada ya Toto kuandika bao pekee la ushindi dakika ya 19 kupitia kwa
mshambuliaji wake, Waziri Junior.
Junior alifunga bao hilo baada ya kuachia shuti kali
akiwa nje ya eneo la hatari baada ya kunasa mpira uliookolewa na mchezaji wa
Simba, Novaty Lufunga.
Wakati Simba ikiendelea kupambana kutafuta nafasi ya
kusawazisha bao hilo, mwamuzi, Ahmada Simba, kutoka Kagera, alimuonyesha kadi
nyekundu na kumtoa nje ya uwanja kocha wa timu hiyo Mganda, Jackson Mayanja,
kwa kumtolea maneno ya kuudhi.
Dakika ya 27, Awadhi Juma, aliikosesha timu yake bao
la wazi baada ya kushindwa kuunganisha vyema kwa kichwa mpira wa krosi ndefu
iliyochongwa na Daniel Lyanga.
Baada ya Mayanja kutolewa, kocha wa makipa wa timu
hiyo, Adam Abdallah, alilazimika kubeba majukumu ya kuliongoza benchi la ufundi
kutokana na kukosekana kwa kocha msaidizi ndani ya kikosi hicho.
Hadi mapumziko Simba walikuwa nyuma kwa bao moja,
ambapo walianza kipindi cha pili kwa kupata pigo jingine baada ya beki, Hassan
Ramadhani ‘Kessy’ kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 46 baada ya kumchezea rafu
mbaya mchezaji wa Toto, Edward Christopher.
Timu hizo ambazo zilikuwa zimekamiana kwa dakika
zote za mchezo, ziliendelea kupambana kwa kasi uwanjani kwa kila mmoja
kushambulia lango la mpinzani wake lakini juhudi hizo hazikuzaa matunda kwa
pande zote.
Baada ya mchezo kumalizika, polisi waliokuwepo
uwanjani walilazimika kupiga mabomu ya machozi ili kuwatawanya mashabiki wa
Simba waliokuwa wakisubiri kulipiga mawe basi la wachezaji.
Mashabiki wa Yanga nao walipigwa mabomu ya machozi
na askari hao baada ya kulizonga basi la Toto wakishinikiza lizimwe ili walisukume
ili kulitoa nje ya uwanja.
Simba: Vicent Angban, Hassan Ramadhani ‘Kessy’,
Mohamed Hussein, Novaty Lufunga, Hassan Isihaka, Jonas Mkude, Peter
Mwalyanzi/Ibrahim Ajibu, Awadhi Juma, Daniel Lyanga, Hamis Kiiza na Mussa
Hassan ‘Mgosi’.
Toto: Musa Kirungi, Erick Mlilo, Salum Chukwu, Yussuf Mlipili, Hassan Khatib, Carlos Protas, Jama
Soudy/Salmin Hozza, Abdallah Seseme, Waziri Junior, Edward Christopher na
Jafari Mohamed/William Kimanzi.


0 comments:
Post a Comment