KAMATI maalumu ya uchunguzi iliyoundwa na Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda imefichua madudu na harufu ya ufisadi
katika utekelezwaji wa mikataba mitatu, inayohusu maeneo ya ukusanyaji mapato
ya Stendi Kuu ya Mabasi Yaendayo Mikoani ya Ubungo na kodi ya uegeshaji magari
katikati ya mji.
Kutokana na madudu hayo, Mkuu huyo wa Mkoa
amebainisha wazi kuwa hataki kufanya kazi tena na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es
Salaam, Wilson Kabwe na Kaimu wake, Sarah Yohana na kuwasilisha majina yao kwa
mamlaka husika ya nidhamu kwa hatua zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam
jana, alisema hivi karibuni aliunda kamati hiyo maalumu kufuatilia maeneo hayo
muhimu kutokana na malalamiko ya muda mrefu, ambayo ofisi yake ilikuwa ikipokea
kutoka kwa wananchi.
Alisema kwa mujibu wa uchunguzi, kamati hiyo
ilibaini kuwa katika stendi ya mabasi ya Ubungo, kumekuwa na ubadhirifu mkubwa
wa fedha za umma, ikiwemo kutokuwasilishwa kwa mapato halisi yanayotokana na
makusanyo ya kila siku serikalini.
“Kamati ile imebaini kuwa pale ubungo kunatumika
sheria ndogo mbili za ukusanyaji mapato moja ya mwaka 2004 na nyingine mwaka
2009 kwa lengo la kunufaisha wachache,” alisema Makonda.
Alifafanua kuwa Sheria Ndogo ya Mwaka 2004 ya
ukusanyaji mapato ndani ya kituo hicho, inaonesha kuwa kila basi linatakiwa
kutozwa Sh 4,000, hivyo makusanyo halisi kwa mwezi ni Sh milioni 42 kutokana na
mabasi 350 yanayoegeshwa kituoni hapo.
Hata hivyo, alisema kutokana na mabadiliko ya tozo,
sheria hiyo ilibadilishwa mwaka 2009 na kila basi likawa linatozwa Sh 8,000 na
hivyo makusanyo ya mwezi yakapanda na kufikia Sh milioni 82 kwa mwezi.
“Lakini cha kushangaza tumebaini kuwa bado kampuni
inayokusanya mapato katika kituo cha Ubungo, inawasilisha mapato hayo kwa
kutumia sheria ya mwaka 2004 yaani Sh milioni 42 badala ya Sh milioni 82 kwa
mwezi…” “…Mbaya zaidi kamati ile katika ukaguzi wake, ilikuta kampuni ya
ukusanyaji mapato hayo stendi ya Ubungo inayo Sheria ya Mwaka 2009 lakini
katika nyaraka za Halmashauri ya Jiji zinaonesha sheria inayotumika ni ya mwaka
2004,” alisisitiza Makonda.
Alisema katika uchunguzi ilibainika kuwa kampuni
iliyo chini ya Halmashauri ya Jiji inayokusanya mapato hayo stendi ya Ubungo,
ilisaini mkataba wa ukusanyaji mapato hayo kwa mara ya kwanza Januari 31, 2004
na baadaye ikasaini tena mkataba Januari 30, mwaka jana.
Kwa mujibu wa Makonda, kwa hali ilivyo tangu Sheria
Ndogo ya Mwaka 2009 ipitishwe, haijawahi kutumika na hivyo kulisababishia
hasara jiji hilo ya Sh bilioni tatu kutokana na mapato katika stendi hiyo
kuendelea kuwasilishwa kwa kutumia sheria ya mwaka 2004.
“Ukipiga hesabu za harakaharaka utagundua kuwa kila
mwezi Sh milioni 42 zimekuwa zikipotelea kwenye mikono ya wachache, kwa maana
hiyo kuanzia mwaka 2009 Sh bilioni tatu zimepotea na kila mwaka tumekuwa
tukipoteza Sh milioni 500, huu ni ufisadi wa aina yake kwa kweli,” alisema.
Alisema wakati fedha hizo zikipotea kwenye mikono ya
wachache, kamati hiyo pia ilibaini kuwa hali ni mbaya katika kituo hicho cha
Ubungo kwani pamoja na ukosefu wa vyoo na maegesho bora kwa mabasi, lakini pia
vibanda vya biashara vilivyomo ndani ya stendi hiyo, vimekuwa vikitumika
kukandamiza maskini na kunufaisha wachache.
“Kwa mujibu wa taratibu, kila kibanda mle ndani ya
stendi kinatakiwa kukodishwa kwa Sh 200,000 kwa mwezi, lakini tumebaini kuwa
wapo watu wachache wamevihodhi na kuvikodisha kwa zaidi ya Sh milioni 1.5,”
alisema.
Kuhusu mkataba wa maegesho katikati ya jiji kupitia
Kampuni ya National Parking System (NPS), alisema kamati hiyo pia imebaini kuwa
Halmashauri ya Jiji imeiongezea mkataba wa miezi 10 kampuni hiyo kinyume cha
taratibu wakati mkataba wake ulikuwa umeshamalizika.
Alisema mara baada ya mkataba huo kumalizika Agosti
mwaka jana Mkurugenzi wa Jiji, Kabwe aliiandikia barua kampuni hiyo na
kuiongezea muda wa miezi sita kwa madai kuwa mchakato wa kutafuta mzabuni mpya
pamoja na kwamba umeanza, haujakamilika.
Aidha, Kaimu Mkurugenzi Yohana naye aliandika miezi
kadhaa baadaye barua na kuiongezea tena kampuni hiyo muda wa miezi minne
iendelee kukusanya kodi ya maegesho kwa kuwa bado mchakato wa kutafuta mzabuni
mpya haujakamilika.
“Barua zote mbili zina saini ya viongozi hawa
wawili, hatua hizi ni kinyume kabisa na maadili ya viongozi pamoja na Katiba ya
nchi. Haiwezekani mchakato wa kumtafuta zabuni uchukue zaidi ya miezi sita,”
alieleza Makonda.
Pamoja na hayo, Makonda pia alisema kamati hiyo
katika uchunguzi wake dhidi ya Kampuni ya Tambaza inayosimamia makosa ya
pikipiki na maegesho ya magari katika sehemu zisizotakiwa, imekuwa ikitoza
fedha nyingi za faini kinyume cha mkataba.
“Mkataba wao unaonesha wazi kuwa wanatakiwa
wakikamata pikipiki yenye makosa watoze faini ya Sh 20,000 lakini imebainika
wao wanatoza zaidi ya Sh 80,000. Licha hivyo pia mkataba unawataka wazingatie
dharura na kutotumia lugha chafu lakini yote haya hawayazingatii,” alisema.
Alisema tangu Rais John Magufuli aingie madarakani
amekuwa mstari wa mbele kupiga vita ubadhirifu wa fedha za umma, rushwa na
ufisadi hivyo akiwa kama Msaidizi wa Rais anaunga mkono juhudi hizo ndio maana
hawezi kunyamazia madudu yeoyote yanayohusu ufisadi.
“Nimewasiliana na mamlaka husika ya nidhamu ili
ichukue hatua stahiki dhidi ya viongozi hawa wawili Kabwe na Yohana na
nimeiambia mamlaka hii kwa uwazi kabisa siwahitaji kuendelea nao hapa Dar es
Salaam,” alisisitiza.
Aidha, alisema tayari amewasiliana na Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuhusu mikataba hiyo yote mitatu
ambayo imeahidi kuanza kuifanyia kazi leo.
Alisema ameamua kuchukua hatua hiyo ya
kuwashughulikia wakurugenzi hao kwa kuwa wao ndio tatizo kwani mikataba hiyo
hata ikivunjwa kwa sasa itakuwa ni kazi bure kama viongozi hao wataendelea
kuwepo.
Hii ni mara ya pili kwa Stendi ya Ubungo kuingia
katika kashfa ya ubadhirifu wa fedha, ambapo mwaka 2011, Waziri Mkuu mstaafu
Mizengo Pinda aliagiza ufanyike uchunguzi, uliobaini kuwepo kwa madudu, hali
iliyosababisha mzabuni aliyekuwepo kuondolewa.


0 comments:
Post a Comment