Sakata la kampuni ya
Lugumi iliyoingia mkataba wa Sh37 bilioni na Jeshi la Polisi wa kufunga mashine
za kielektroniki za kuchukua alama za vidole nchi nzima, sasa limetua Takukuru
baada ya taasisi ya kupambana na rushwa kuchukua faili lake la usajili.
Kampuni hiyo
ilibainika kutotimiza matakwa ya mkataba wake baada ya kufunga mashine 14 tu
kati ya 108 ilizotakiwa kufunga, licha ya kulipwa asilimia 99 ya fedha kwa mujibu wa mkataba.
Ripoti ya Mkaguzi na
Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) ya mwaka 2013/14 ndiyo iliyofichua udhaifu huo.
Wakati Kamati ya
Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ikitaka nguvu itumike ili Jeshi la Polisi
liwasilishe mkataba huo, utata umeibuka katika umiliki wa kampuni hiyo kutokana
na kuwepo tuhuma kuwa baadhi ya vigogo wa Polisi na wanasiasa ni wanahisa wa
Lugumi Enterprises.
Jana, Ofisa Mtendaji
Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), Frank Kanyusi alisema
kuwa Takukuru inashughulikia suala hilo, huku akibainisha kuwa kwa sasa Brela
hawana takwimu za kina za kampuni hiyo.
“Kampuni hii
ilisajiliwa kihalali na kupewa cheti cha usajili. Ila ninachoweza kukueleza kwa
sasa ni kwamba jalada la usajili la Lugumi lipo Takukuru kwa ajili ya uchunguzi
zaidi,” alisema Kinyusi jana.
Kanyusi, ambaye
hakutaka kuzungumzia kiundani kuhusu usajili wa kampuni hiyo, alisema:
“Waandishi wa habari wamekuwa wakiniuliza maswali mengi kuhusu suala hili ila
kwa sasa hali ndiyo hiyo. Jambo hili lipo Takukuru.”
Alisema kwa sasa
kampuni zilizosajiliwa na Brela zipo 120,000 na zinakaribia kufika 130,000 na
kwamba kampuni lazima zitoe taarifa zake kila mwaka, kinyume na hapo zinaweza
kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kufutwa.
Habari za uhakika
kutoka ndani ya Brela zilieleza kuwa
taarifa za usajili wa kampuni hiyo zilitoweka takribani miezi miwili iliyopita.
Mwandishi alipofika katika ofisi za wakala huyo kwa
ajili ya kupata ukweli wa usajili, alielezwa na mmoja wa watumishi ambaye
hakutaka jina lake kuwekwa wazi kwamba ni vigumu kupata hilo jalada kwa sababu
ya mvutano ulioibuka.
Hata baada ya
kufuata taratibu za kupewa jalada hilo kwa ajili ya kupitia masuala mbalimbali,
alijibiwa kuwa jalada hilo halionekani ingawa baadaye Kanyusi alisema
limechukuliwa na Takukuru.
Sakata la Lugumi
liliibuka wiki iliyopita wakati PAC ilipokutana na Jeshi la Polisi kupitia
taarifa ya hesabu zao za mwaka 2013/14 zilizokaguliwa na CAG.
Katika hesabu hizo
ilibainika kuwa mwaka 2011, Polisi iliingia mkataba na Lugumi kwa ajili ya
kufunga mashine hizo katika vituo 108 vya polisi kwa gharama ya Sh 37 bilioni.
Hata hivyo,
ilibainika kuwa kampuni hiyo imefunga mitambo hiyo kwenye vituo 14 tu, huku
ikilipwa asilimia 99 ya fedha hizo.
Kutokana na ukakasi
huo, PAC ambayo ilibaini viashiria vya ufisadi katika mkataba huo, iliagiza
watendaji wa Polisi kuwasilisha taarifa za mkataba huo pamoja na vielelezo
vyake ili kamati hiyo iweze kuupitia na kujiridhisha.
Lakini hadi sasa
Jeshi la Polisi halijawasilisha mkataba huo, jambo ambalo huenda likazua
mjadala mkali katika mkutano wa Bunge unaoanza Jumanne ijayo.


0 comments:
Post a Comment