ALIYEKUWA Mkuu wa
Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela, ameibukia kanisani na kutoa ya
moyoni, ikiwa siku tano baada ya Rais Dk. John Magufuli kutengua uteuzi wake.
Kilango, ambaye
Jumatatu wiki hii uteuzi wake ulitenguliwa baada ya Machi 20, mwaka huu, kudai
kuwa mkoa wa Shinyanga hauna mtumishi hewa wa serikali hata mmoja.
Hata hivyo, Ikulu
ilifanya uchunguzi na kubaini kuwa katika taarifa za awali kuna watumishi hewa
45, huku kazi ya uhakiki ikiendelea katika wilaya za Ushetu na Shinyanga.
Rais Magufuli
aliwaagiza wakuu wa mikoa wote, alipokuwa akiwaapisha kuwa wafanya uchunguzi
kuhusu uwapo wa watumishi hewa katika mikoa yao na kutoa taarifa.
Kutokana na kutoa taarifa
hizo zisizo za kweli, Jumatatu wiki hii, Rais Magufuli alitangaza kutengua
uteuzi wake, akiwa amekaa kwenye nafasi hiyo kwa siku 27. Kilango amekuwa mkuu
wa mkoa wa 19 tangu kuanzishwa kwa mkoa huo.
Mbali na Kilango,
Rais Magufuli pia alimsimamisha kazi Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Abdul
Dachi, kutokana na taarifa hizo za kutokuwapo watumishi hewa katika mkoa.
ALIYOSEMA KANISANI.
Akiwasalimia waumini
wenzake juzi, katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi
ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria, mjini Shinyanga, baada ya kupewa fursa ya
kusema neno, Kilango alisema anamshukuru Mungu kwa kila jambo kwa yote
yaliyomtokea.
“Ndugu waumini
wenzangu, hili ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu. Hata mtu unapojifungua
mtoto akafariki dunia, unamshukuru Mungu kwani hayo ni mapenzi ya Mungu.
“Ukiona mzazi wako
kafariki dunia pia, unamshuruku Mungu. Tunao wajibu wa kumshukuru Mungu kwa
kila jambo,” alisema kwa maneno mafupi na kisha kuketi, huku akiacha simanzi
miongoni mwa waumini wenzake, wakiwamo viongozi wa kanisa.
ALIVYOANZA KAZI
Mbele ya kikao cha
Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), muda mfupi baada ya kuanza kazi, Kilango
alisema Shinyanga ni mkoa wenye changamto nyingi ambazo atazishughulikia,
lakini atakuwa akilazimika kukimbia Dar es Salaam kumwona mwenzi wake, Mzee
John Malecela ambaye ni mgonjwa, na pindi hali yake ikiimarika wataungana naye
mjini Shinyanga.
Hayo aliyasema Machi
22, mbele ya wajumbe wa kikao cha kamati hiyo na Ijumaa Machi 25, alisali
kanisani hapo.
Sambamba na hayo,
aliahidi kupambana na watumishi wazembe na wale wanaoendekeza rushwa na ufisadi
na kurejesha hadi ya mkoa wa Shinyanga kimaendeleo.
Kilango ambaye yuko
mjini Shinyanga, akisubiri kukabidhi ofisi kwa mrithi wake kwa mujibu wa
utaratibu, bado anaishi hotelini kwa vile aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Ally
Rufunga, hajaondoka katika nyumba ya serikali iliyoko Ikulu ndogo, eneo la
Lubaga.
ALICHOKISEMA
MAGUFULI.
Wakati akipokea
hundi ya Sh. bilioni sita kutoa kwa Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tilia Ackson,
Rais Magufuli alisema aliwapa wakuu wa mikoa siku 15 wakasimamie watumishi
hewa, ambazo zilimalizika Machi 31, mwaka huu.
Alisema katika siku
hizo 15, aliwaruhusu kufanya kazi hiyo kwa uhuru na kuwaahidi hakutatokea kitu
chochote na kwamba walifanya kazi vizuri.
Rais Magufuli
alisema watumishi hewa waliopatikana ni 5,507 ambao walikuwa wanalipwa
mishahara na miongoni mwao walikuwamo wanafunzi, waliokufa na waliofungwa.
Alisema serikali
imekuwa ikitenga Sh. bilioni 583 kulipa mishahara na kati ya fedha hizo hulipwa
watumishi hewa.
“Ninaamini uchambuzi
utaendelea kufanyika ili kuokoa mabilioni ya fedha. Wizara ya Utumishi na ya
Fedha muendelee kufanya kazi hiyo,” alisema Magufuli.
Alisema zaidi ya Sh.
bilioni 53 zilikuwa zinapotea kwa kuwalipa watumishi hewa 5,507.
Rais Magufuli
alisema watumishi hewa hawako katika halmashauri tu, bali wako kila idara ya
serikali, zikiwamo Ofisi ya Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu, vyombo vya ulinzi na
usalama, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na hata
Wizara ya Fedha na Mipango.
Alisema wakati
akiwaapisha wakuu wa mikoa kwa kutambua tatizo hilo kuwa ni kubwa, aliwapa
agizo hilo na wengi waliitikia wito na kufanya kwa ufanisi.
Rais Magufuli
alisema akiwa wilayani Chato, aliona taarifa zikitolewa na wakuu wa mikoa
kuhusu watumishi hewa, lakini alishangaa kusikia Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga
(Kilango), akisema katika mkoa wake hakuna mtumishi hewa hata mmoja.
“Nilijiuliza ni
kweli? Nikatoa maagizo nikiwa Chato kuwa watu waende ‘ku-verify’ (kuthibitisha)
katika kila wilaya kama kweli hakuna watumishi hewa. Hadi jana usiku (Jumapili
usiku) walipatikana watumishi hewa 45 na bado wilaya mbili zilikuwa
hazijahakikiwa,” alisema.
“Niilijiuliza sana,
nikajiuliza sana na kweli nilijuliza maswali mengi kwa masikitiko mengi kwa
nini mkuu wa mkoa alizungumza vile wakati hakukuwa na adhabu yoyote, lengo lake
lilikuwa nini?
“Je, kama ni mkuu wa
wilaya au wasisidizi wake walimdanganya kwa nini na yeye alidanganya, ni
shetani gani aliyemkumba? “Nimeamua nitengue uteuzi wa mkuu wa mkoa wa
Shinyanga na atapangiwa kazi nyingine pamoja na katibu tawala wa mkoa,” alisema
Magufuli.
CHANZO: NIPASHE.


0 comments:
Post a Comment