KAMPUNI ya Symbion Power ya mjini Washington
Marekani imesema kwamba haikuilipa Kampuni ya Rental Services and Solutions
(RSS) fedha wanazodai kwa kuwa wametumia fedha hizo kulipa kodi baada ya
kampuni ya Dubai kukimbia nchini bila kulipa kodi kwa Serikali.
Taarifa iliyotolewa juzi kwa vyombo vya habari
ilieleza kuwa kampuni ya RSS ambayo ilikuwa inafanya kazi nchini kama mshirika
wa Symbion kwa miaka mitatu kuanzia 2011 hadi 2014, katika muda huo hawakulipa
hata dola moja kwa Serikali ya Tanznaia kinyume inavyotakiwa kwa mujibu wa
sheria.
Taarifa iliyomkariri Makamu wa Rais Mwandamizi wa
Symbion anayehusika na Kitengo cha Mawasiliano na Masuala ya Kijamii, Adi Raval
akisema “Kiuhalisia hili ni suala la kodi. Hii kampuni iitwayo RSS na washirika
wake walikuwa wakifanya kazi kama makandarasi waliokamishwa na Kampuni ya
Symbion kwa miaka mitatu.
“Kutoka mwaka 2011 mpaka mwaka 2014. Katika muda huo
hawakulipa hata dola moja ya kodi kwa Serikali ya Tanzania kinyume cha inavyotakiwa
kwa mujibu wa sheria.”
Aliongeza kuwa RSS na washirika wake walibaki nchini
Tanzania wakiwa na wataalamu wao katika miji ya Arusha, Dodoma na Dar es Salaam
na sheria iliwataka walipe kodi lakini kwa makusudi hawakufanya hivyo.
“Tumekata kodi kwenye malipo yao na kuilipa Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA). Tutawalipa fedha nyingine iwapo wataweza kutoa
uthibitisho wa cheti kikionesha kuwa tayari wamelipa kodi kwa TRA,” alisema
Raval.
Alipotakiwa kuthibitisha madai hayo ya ukwepaji
kodi, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo
alisema hawezi kuthibitisha au kukanusha madai hayo ya ukwepaji kodi
yanayodaiwa kufanywa na kampuni ya RSS hadi hapo watakapofanya uchambuzi wa
nyaraka mbalimbali kuhusu kampuni hizo.
Juzi kwenye vyombo vya habari kulikuwa na habari
kuwa Kampuni ya Rental Solutions and Services LLC inaidai Kampuni ya Symbion
Tanzania Ltd Sh bilioni 560 kama fidia na malipo ya ukodishaji wa mitambo ya
kuzalishia umeme nchini.
0 comments:
Post a Comment