Tanzania inaungana na Mataifa mengine duniani kuadhimisha
Siku ya Malaria Aprili 25 Mwaka huu ili kutathmini mafanikio ya utekelezaji wa
mikakati mbalimbali ya kupambana na
ugonjwa huo hapa nchini.
Mkuu wa wilaya ya Ilala Bw. Raymond Mushi
akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam juzi kuhusu maadhimisho
ya Siku ya Malaria Duniani jijini Dar es salaam amesema maadhimisho ya mwaka
huu yanalenga kuwakumbusha na kuwaelimisha wananchi juu ya athari za ugonjwa wa
Malaria na mbinu za kukabiliana na ugonjwa huo.
Alisema kuwa maadhimisho hayo kitaifa yatafanyika
katika viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam chini ya kauli mbiu isemayo
Wekeza kwa Maisha ya Baadaye, Tokomeza Malaria huku msisitizo mkubwa ukilenga
kuikumbusha na kuielimisha jamii kuepuka athari na madhara yanayotokana na ugonjwa huo
Bw. Mushi amesema maadhimisho ya mwaka huu yamelenga kuwaelimisha wananchi juu ya
umuhimu wa kutambua dalili za malaria na kuwahi kwenye vituo vya kutolea huduma
pindi wasikiapo dalili za ugonjwa huo ili waweze kupima afya zao na kupatiwa matibabu.
“Ugonjwa wa malaria kwa muda mrefu umekuwa na athari
kwa nguvu kazi ya taifa na utekelezaji wa mikakati mbalimbali, hivyo ni wajibu
wetu kushirikiana kuwaelimisha wananchi kuwahi katika vituo vya afya pindi
wasikiapo dalili za malaria” Amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Uhamasishaji
Mpango wa Udhibiti wa Maambukizi ya Malaria Dkt. Linda Nakara akizungumza
kuhusu maadhimisho hayo amesema kuwa maadhimisho ya mwaka huu yataambatana na
wadau mbalimbali wa huduma za afya kufanya maonyesho ya huduma wanazotoa kwa
jamii.
Ameongeza kuwa wadau hao pia wataendesha shughuli za
uchunguzi wa vimelea vya malaria kwa kutumia vipimo vinavyotoa majibu kwa
haraka (MRDT) na matibabu ya ugonjwa wa malaria kwa wale watakaogundulika kuwa
na malaria.
Mkuu wa wilaya ya Ilala Bw. Raymond Mushi
akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam kuhusu maadhimisho ya
Siku ya Malaria Duniani mwaka 2015 alipokutana na waandishi wa habari leo
jijini Dar es salaam. Maadhimisho ya mwaka huu yanalenga kuwakumbusha na
kuwaelimisha wananchi juu ya athari za Malaria na mbinu za kukabiliana na
ugonjwa huo.
0 comments:
Post a Comment