JUZI Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda
alisisitiza nia yake ya kutaka kulifanya Jiji la Dar es Salaam kuwa bora katika
suala la usafi, utulivu na amani kwa ujumla.
Alisema amejipanga kuanza na mambo matatu, la kwanza
likiwa kuwaondoa ombaomba wa barabarani, kuwabana wamiliki wa majengo makubwa
yaliyojengwa kinyume na taratibu pasipokuwa na sehemu za kuegesha magari na
kuwaamuru wamiliki wa baa kutopiga muziki nje ya utaratibu wa vibali vyao.
Mikakati hiyo imekuwa baada ya ule wa awali wa
kuwataka wakazi wa jiji hilo kuhakiki silaha zao ndani ya miezi mitatu, kabla
ya kuanza msako, lengo likiwa ni kuhakikisha matukio ya uhalifu yanapungua na
ikiwezekana yanatoweka Dar es Salaam.
Kwa hakika, tunaungana na juhudi zenye nia njema
zinazofanywa na Mkuu wa Mkoa katika kuhakikisha Dar es Salaam inakuwa mahali
salama pa kuishi. Tukianza na hili la ombaomba, ni ukweli usiofichika kwamba
kwa muda mrefu wamegeuka kero katika jiji hilo ambalo ni sura ya nchi kutokana
na kuwa na shughuli nyingi za kiuchumi na kiutawala.
Mbali ya kuchafua mazingira katika maeneo mbalimbali
ya mji wanayoyageuza kuwa makazi, ikiwa ni pamoja na majengo na ofisi za umma
katikati ya Jiji, vituo vya mabasi, kwenye makutano ya barabara na kadhalika,
ombaomba wanatajwa pia kuwa mawakala wa wahalifu.
Wanatajwa kushirikiana kwa kiasi kikubwa na wahalifu
nyakati za usiku, lakini pia ombaomba hao wanatumika katika biashara haramu,
zikiwemo za kusambaza dawa za kulevya. Na wakati mwingine, baadhi ya vijana
ambao mchana huonekana kama wenye shida za kweli na hivyo kustahili kusaidiwa
angalau mkono uende kinywani, hugeuka vibaka hatari katika maeneo mengi ya
katikati ya mji.
Hivyo basi, tunaamini hatua ya kuwaondoa watu wa aina
hii ambao baadhi yao huelezwa hugeuka ma`pedeshee’, itasaidia harakati za
kuliweka jiji katika hali ya usafi, lakini pia ni sehemu ya mkakati wa
kupunguza matukio ya kihalifu.
Aidha, katika kuhakikisha Dar es Salaam inakuwa na
utulivu na amani nyakati za usiku, suala la udhibiti wa kelele katika kumbi za
starehe na kwenye baa, nalo lina uzito mkubwa, kwani ni moja ya kero kwa wakazi
wa jiji hilo.
Wengi wa wamiliki wake hupiga muziki kwa sauti
kubwa, tena kwa zaidi ya saa zilizowekwa kisheria, hivyo kuathiri kwa kiasi
kikubwa wakazi katika maeneo husika, tena bila ya vibali vya kufanya hivyo.
Mbali ya kusababisha usumbufu kwa wakazi wa Jiji
karibu siku zote za wiki, maeneo haya hugeuka pia maficho ya wahalifu. Hivyo,
tunaamini ni sahihi wahusika wakibanwa ili wafanye shughuli zao ndani ya wakati
unaokubalika kwa mujibu wa sheria.
Ndiyo maana tunasema kwa haya machache anayoanza
nayo Mkuu wa Mkoa, ni vyema akaungwa mkono ili kumsaidia kurudisha hadhi ya
Jiji la Dar es Salaam katika suala la usafi, amani na utulivu.


0 comments:
Post a Comment