MBUNGE wa Jimbo la Ubungo, Saed Kubenea (Chadema)
amehukumiwa kifungo cha miezi mitatu baada ya kupatikana na hatia ya kutumia
lugha ya matusi.
Kubenea amehukumiwa ad habu hiyo jana baada ya
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kumtia hatiani katika kosa la kumtukana
aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa
wa Dar es Salaam.
Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi wa Mahakama
hiyo, Thomas Simba alikubaliana na ombi la mshitakiwa huyo na kumhukumu adhabu
ya kukaa nje miezi mitatu bila kujihusisha na kosa kama hilo.
“Nakubaliana na maombi ya mshitakiwa aliyotoa
mahakamani hapa, hivyo anastahili kupewa adhabu ya huruma na mahakama inampa
adhabu ya kukaa nje kwa muda wa miezi mitatu bila kujihusisha na kosa kama
hili,” alisema Hakimu Simba.
Pamoja na adhabu hiyo, mshitakiwa Kubenea pia
atasaini karatasi ya mahakama ambayo inaonesha kukubali kwa adhabu hiyo.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Simba alisema mshtakiwa huyo ametiwa hatiani baada
ya mahakama kujiridhisha na ushahidi wa mashahidi watatu kutoka upande wa mashitaka
waliotoa mahakamani hapo.
Alisema katika ushahidi wake, shahidi namba moja
katika kesi hiyo, Makonda alidai Desemba 14, 2015 katika kiwanda cha TOOKU
Garments Co. Ltd kilichopo Mabibo External, Kubenea akimtolea lugha chafu kuwa
ni kibaka, mjinga, mpumbavu na kwamba nafasi yake ni ya kupewa.
Alisema baada ya kuchunguza ushahidi wa pande zote
mbili, mahakama imethibitisha pasi na kuacha shaka kuwa maneno hayo yangeleta
uvunjifu wa amani, na hivyo mahakama ilimtia hatiani kwa lugha ya matusi.
Hata hivyo upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili
wa Serikali, Mtalemwa Kishenyi ulidai mahakamani hapo kuwa hauna kumbukumbu za
nyuma kuhusu hatia za mshtakiwa.
Kabla ya kupewa kwa adhabu hiyo, Kubenea aliiomba
mahakama hiyo impe adhabu nafuu, ambayo itamfanya aendelee kuhudumia wananchi
wake. Kubenea alijitetea kuwa bado wananchi wake wanahitaji awahudumie kwa kuwa
ni mbunge wa Ubungo na pia upande wa Jamhuri, umekiri kuwa hana rekodi ya
mashtaka, hivyo aliomba mahakama hiyo impunguzie adhabu.
“Mimi nilienda katika kiwanda hicho kwa ajili ya
kutatua mgomo uliokuwepo baina ya wafanyakazi na uongozi wa kiwanda hicho na
kulikuwa hakuna uvunjifu wa amani kama jinsi ilivyoripotiwa, ” alidai Kubenea
na kuongeza; “Naiomba mahakama yako inipe adhabu nafuu ambayo nitaweza
kuwatumikia wananchi wangu.”
Hata hivyo kutokana na maombi hayo , hakimu Simba
alisema kesi kama hiyo, hukumu yake inaweza kuwa ni faini au kwenda jela bila
faini au mahakama inaweza kumuachia bila masharti yoyoye .


0 comments:
Post a Comment