RAIS John Magufuli jana alizindua rasmi ujenzi wa
barabara ya juu (flyover) katika makutano ya Tazara jijini Dar es Salaam. Rais
alisema ujenzi wa barabara hiyo ya juu unaotarajiwa kuanza karibuni,
utakamilika Oktoba 2018 na kugharimu Sh bilioni 100 za Tanzania.
Rais alitamani kuona ujenzi huo unakamilika hata
kabla ya muda huo na sisi tunawasihi makandarasi kujitahidi ili hilo
liwezekane. Rais pia alitaja miradi mingine inayotazamiwa kujengwa ikilenga
kuondoa kero za msongamano katika jiji hilo kuwa ni pamoja na kukamilika kwa
daraja la Kigamboni ambalo litazinduliwa rasmi keshokutwa, Jumanne, ujenzi wa
barabara ya kutoka Kigamboni hadi Chalinze, pamoja na barabara nyingine ya juu
itakayojengwa Ubungo.
Miradi mingine inayokuja ni wa daraja litakalopita
kando ya bahari kuanzia Koko Beach hadi Aga Khan, ujenzi wa Reli ya Kati
utakaosababisha magari makubwa kutoingia tena katikati ya jiji pamoja na ukamilishaji
wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART).
Kama alivyosema Rais, miradi hiyo itaibadilisha Dar
es Salaam ambapo mbali na kupunguza kero za msongamano itaipa sura mpya Dar es
Salaama na kuifanya kuwa mahali salama zaidi kama lilivyo jina lake. Aidha,
Rais Magufuli alisema miradi hiyo pia itatengeneza ajira kwa Watanzania.
Tunaipongeza Serikali ya Awamu ya Tano, kwa kuanza
kutekeleza mradi huo wa ujenzi wa barabara ya juu Tazara na mingine inayokuja,
hatua inayodhihirisha kwamba ahadi za Rais Magufuli alizozitoa wakati akiomba
kura mwishoni mwa mwaka jana ni za kweli na zitatekelezeka.
Kupunguza, kama si kuondoa kabisa kero ya msongamano
jijini Dar es Salaam ni hatua muhimu kutokana na faida zake nyingi zikiwemo za
kiuchumi kwa kuwa muda mwingi sana wa uzalishaji umekuwa ukipotea kwenye foleni
sambamba na mafuta mengi yanayotumiwa na magari katika eneo fupi.
Wakati Serikali kwa upande wake ikidhamiria
kutekeleza miradi hiyo muhimu, sisi wananchi kwa upande wetu tunatakiwa tuwe
tayari kuisaidia ili ikamilishe malengo yake ambayo yana faida kubwa kwetu
tunaoishi sasa na hata vizazi vijavyo.
Mambo ya kuisaidia mengi lakini kubwa, kama
alivyosema Rais Magufuli, ni kulipa kodi. Bila kulipa kodi, hakuna ubishi
kwamba miradi mingi tunayoitarajia kuwa chachu ya mendeleo ya nchi yetu itabaki
kuwa ndoto.
Na kwa kweli hatuna sababu ya kukwepa kulipa kodi
kwani matumizi yake tunayaona. Lingine ni kuwa waangalifu kwa kutunza
miundombinu hii tunayojengewa na serikali yetu. Ni vyema pia watakaobahatika
kupata ajira kwenye ujenzi wa miundombinu hii, wakamsikia Rais alivyowaasa;
kuacha vitendo vya wizi wa vifaa kwa manufaa ya Taifa.


0 comments:
Post a Comment