KAMATI ya Waamuzi wa Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), imesema kuwa haikubaliani na maamuzi ya Kamati ya Nidhamu ya
kuwasimamisha waamuzi waliochezesha mechi za mwisho za Ligi Daraja la Kwanza
kati ya JKT Kanembwa FC dhidi ya Geita Gold na Polisi Tabora dhidi ya JKT
Oljoro.
Pia kamati hiyo ipo tayari kuwasaidia waamuzi hao
waliosimamishwa wakituhumiwa kupanga matokeo iwapo watakuwa tayari kukata
rufaa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi,Salum Chama, alisema
kuwa wakati suala hilo likifanyiwa uchunguzi na Kamati ya Nidhamu, hakuna
mwamuzi yeyote mkongwe au aliyekuwepo katika kamati yao aliyeitwa ili kutafsiri
mipaka na kanuni za kazi zao.
Alisema wao kamati ya waamuzi wamekuja kusikia
maamuzi yakitolewa pasipo kushirikishwa jambo ambalo halipo kisheria lakini pia
maamuzi yaliyotolewa hayakuwa na haki kwani hakuna ushahidi wa kutosha
uliowakamatisha waamuzi hao.
“Kuanzia mwanzo hadi mwisho wa sakata lile hakuna
aliyeshirikishwa katika kamati yetu, jambo ambalo kwa upande fulani si haki
kwani na sisi tuna sheria na kanuni zetu ambazo tunazitumia uwanjani, lakini
pia hadi hivi sasa hakuna ushahidi wa kutosha ni vipi wamekutwa na tuhuma za
upangaji matokeo.
“Sisi kamati ya waamuzi, tupo tayari kuwasimamia
bega kwa bega iwapo kama wenyewe wanaona
hawakutendewa haki na wakakata rufaa, lakini wakiomba tuwasimamie katika hilo
tupo tayari,” alisema Chama.
Hivi karibuni Kamati ya Nidhamu ya TFF chini ya
Makamu Mwenyekiti wake Wakili, Jerome Msemwa, iliwafungia maisha kutojihusisha
na mpira wa miguu mwamuzi wa mchezo kati ya JKT Kanembwa FC v Geita Gold, Saleh
Mang’ola, kamisaa wa mchezo huo, Moshi Juma pamoja na mwamuzi wa mchezo kati ya
Polisi Tabora dhidi ya JKT Oljoro, Masoud Mkelemi na mwamuzi wa akiba, Fedian
Machunde, waliofungiwa kwa muda wa miaka kumi
pamoja na kutozwa faini ya shilingi milioni kumi kila mmoja baada ya
kukutwa na hatia ya upangaji matokeo kwenye michezo hiyo.


0 comments:
Post a Comment