Image
Image

UKAWA wakataa kuchangia Mjadala wa Hotuba ya waziri Mkuu.


KIONGOZI wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, jana aligoma kuwasilisha maoni ya kambi hiyo akitoa hoja tatu zilizosababisha kuchukua uamuzi huo ambazo pia zinaweza kuwa chanzo cha wao kususia bajeti.
Hoja hizo ni Serikali ya Rais Dk. John Magufuli kufanya kazi bila ya kuwa na mwogozo wowote wenye msingi halali wa kisheria katika wizara zake, uvunjaji wa Katiba na sheria za nchi kuhusiana na Bajeti na Serikali kupoka madaraka na uhuru wa mhimili wa Bunge.
Katika hilo, Mbowe alilieleza Bunge kuwa Kambi ya Upinzani Bungeni haitakuwa tayari kuendelea kushiriki uvunjaji wa Katiba, Sheria na haki za msingi za wananchi na kwamba wanatafakari kwa kina na makini hatua za kufuata.
SERIKALI KUTOKUWA NA MWONGOZO.
Mbowe ambaye alikuwa akiwasilisha taarifa ya Kambi ya Upinzani wakati wa kipindi cha jioni, alisema kutokana na kukosekana kwa mwongozo halali wa kisheria katika wizara za Serikali ya Rais Magufuli, inaonyesha kiongozi huyo hajaiunda kihalali Serikali yake.
Akifafanua hilo Mbowe alisema kiongozi huyo wa nchi ameshindwa kutekeleza sheria ya utekelezaji wa majukumu ya mawaziri ya mwaka 1980, ambayo inaweka masharti ya kutengeneza mwongozo wa muundo na utekelezaji wa majukumu ya Serikali yake.
Alisema sheria hiyo pamoja na mambo mengine kila linapotaka kuundwa Baraza la Mawaziri inamtaka rais kuchapisha katika gazeti la Serikali kueleza jinsi Serikali yake itakavyotekeleza majukumu yake, jambo ambalo halijafanyika na badala yake Serikali imekuwa ikifanya kazi kwa kauli za rais na mawaziri bila kufuata mwongozo wowote.
“Sheria ya Utekelezaji wa majukumu ya mawaziri ya mwaka 1980, kifungu cha 5(1) kinaweka masharti kwa rais kutengeneza mwongozo wa muundo na utekelezaji wa majukumu ya Serikali yake.
“Mpaka sasa mwongozo wa utendaji wa Serikali kwa kila wizara (Instrument) unaotumika ni ule uliochapishwa kwenye gazeti la Serikali namba 494A la tarehe 17/12/2010. Kwa mujibu wa Instrument hiyo, majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu ni Coordination of Government Business, Leader of Government Business in the National Assembly, Link between Political Parties and Government, National Festivals and Celebration of Management of Civic Contingencies (relief).
“Mheshimiwa Spika, kitendo cha Serikali hii kuendesha kazi zake kwa mwongozo wa 2010, ina maanisha kwamba majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu bado ni yale yale yaliyochapishwa mwaka 2010, kwa sababu gazeti hilo la Serikali halijafutwa,” alisema Mbowe huku akishangiliwa na wabunge wa upinzani.
UVUNJAJI WA KATIBA/SHERIA KUHUSU BAJETI
Mbali na hilo la mwongozo, Mbowe alieleza jinsi Serikali ambavyo imekuwa ikivunja Katiba na sheria za nchi kwa kufanya matumizi ya fedha ambazo hazikuidhinishwa na Bunge.
Huku akiitolea mfano Wizara ya Ujenzi iliyokuwa ikiongozwa na Magufuli mwenyewe kabla hajachaguliwa kuwa rais, kwa kufanyiwa matumizi ya fedha kinyume na yale yaliyoidhinishwa na Bunge, Mbowe alinukuu vifungu vya Katiba ibara ya 63(3)(b), vinavyoeleza mamlaka ya Bunge kujadili utekelezaji wa kila wizara wakati wa Mkutano wa Bunge wa kila mwaka wa Bajeti na kuidhinisha Bajeti ya Serikali.
“Utaratibu huo wa kisheria umekuwa ukivunjwa na Serikali kwa kufanya matumizi ya fedha ambazo hazikuidhinishwa na Bunge jambo ambalo linaua dhana ya madaraka ya Bunge ya kuisimamia na kuishauri Serikali.
“Ili kuthibitisha jambo hilo, kwa mfano bajeti ya maendeleo iliyokuwa imeidhinishwa na Bunge kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka wa fedha 2015/16 ilikuwa ni shilingi bilioni 883.8 ambapo kati ya fedha hizo, fedha za ndani zilikuwa ni shilingi bilioni 191.6,” alisema.
Akifafanua katika hilo, Mbowe alisema ikiwa fedha zilizoidhinishwa na Bunge hazikutosha kutekeleza majukumu ya Serikali, kifungu cha 41(1) cha Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015 kinaelekeza kwamba, Serikali itawasilisha bungeni kwa idhini, bajeti ya nyongeza ya fedha zilizotumika ambazo zimezidi kiwango kilichoidhinishwa na Bunge au kwa madhumuni ya kugharamia mahitaji ambayo hayakupangwa.
“Mheshimiwa Spika, utaratibu huu unatiliwa nguvu na Sheria ya Fedha za Umma wa mwaka 2001( Public Finacne Act, 2001), ambapo kifungu cha 18 (3) na (4) kinaitaka Serikali kuleta bungeni bajeti ya nyongeza ( mini-budget) kwa ajili ya kupata idhini ya Bunge ikiwa fedha zilizoidhinishwa awali hazikutosha.
Akitolea mfano wizara hiyo ya ujenzi ambayo alisema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016 iliyokuwa imeidhinishiwa na Bunge, kiasi cha shilingi bilioni 883.8 ambapo kati ya fedha hizo za ndani zilikuwa shilingi bilioni 191.6 lakini cha kushangaza ilipokea kutoka Hazina kiasi cha shilingi bilioni 607.4 kama fedha za ndani.
“Kitendo cha Serikali kuamua kufanya re-allocation ya bajeti bila kupata idhini ya Bunge ni dharau kwa Bunge, lakini mbaya zaidi ni uvunjaji wa Katiba na Sheria,” alisema.
UHURU WA BUNGE
Akizungumza uhuru na madaraka ya Bunge, Mbowe alipinga kitendo cha chombo hicho kupokwa mamlaka yake iliyopewa na wananchi kutokana na hatua ya Serikali kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya mikutano yake.
“Bunge ni chombo cha uwakilishi wa wananchi na wananchi wana haki ya kujua Bunge lao linavyofanya kazi ili wawe na uwezo wa kuwawajibisha wawakilishi wao iwapo hawafanyi kazi inavyostahili.
Katika hali isiyo ya kawaida, Serikali na uongozi wa Bunge imewapoka wananchi haki yao ya kupata habari za Bunge kwa kuzuia mijadala bungeni kurushwa moja kwa moja na televisheni ya Taifa na vyombo vingine vya habari vya kujitegemea.
“Jambo hili pia ni uvunjwaji wa ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo inasema kwamba kila mtu anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake; anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi, anao uhuru wa kufanya mawasiliano na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano yake na anayo haki ya kupewa taarifa wakati wowote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii,” alisema Mbowe.
HALI ILIVYOKUWA
Baada ya Mbowe kuwasilisha taarifa yake hiyo alitoka nje na kuzungumza na waandishi wa habari huku akiwa ameambatana na wabunge kadhaa wa Ukawa akiwemo Mbunge wa Vunjo, James Mbatia, Mbunge wa Viti Maalumu Severina Mwijage, Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya wote wa CUF, Mbunge wa Momba, David Silinde, Mchungaji Peter Msigwa pamoja na Mbunge wa Viti Maalumu, Devitha Minja wote wa (Chadema).
Kauli ya Chenge
Akizungumza baada ya Mbowe kuwasilisha hoja hiyo, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, alisema hotuba ya Mbowe imebeba maneno mazito ya kutuhumu moja kwa moja kwamba kuna uvunjwaji wa Katiba ya nchi jambo ambalo si sawa.
Chenge alisema wenye wajibu wa kutafsiri sheria au katiba inavunjwa si wao bali ni mahakama, hivyo akawataka wafuate utaratibu wa kupeleka hoja zao huko.
Alisema kilichofanywa na Mbowe ni kuwatoa kwenye reli kwani mjadala ulikuwa ni hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
“Huu walioufanya si utaratibu sahihi wa kuwasilisha hoja zao, walipaswa kufuata utaratibu wa kisheria,” alisema Chenge.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment