Maafisa usalama wa Libya wanaolinda visima vya
mafuta nchini humo wamelazimika kufunga visima vitatu vya mafuta kutokana na
wafanyakazi katika visima hivyo kugoma kwenda kazini kwa kuhofia mashambulio ya
genge la kigaidi la Daesh.
Shirika la habari la Reuters limeripoti kutoka mjini
Benghazi kuwa, hivi sasa kumeenea wasiwasi nchini Libya kuwa, kundi la kigaidi
la Daesh litadhibiti visima vya mafuta vya nchi hiyo na kusababisha hasara
kubwa za mali na roho kwa wananchi wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Hii ni katika hali ambayo katika miezi ya hivi
karibuni, kundi la kigaidi la Daesh limekuwa likifanya mashambulizi ya mara kwa
mara katika visima vya mafuta vya nchi hiyo, ingawa limeshindwa hadi hivi sasa
kudhibiti maeneo hayo.
Uzalishaji wa mafuta nchini Libya umepungua mno hivi
sasa. Kiwango hicho ni cha chini ya khumusi moja ya kiwango kilichokuwa
kikizalishwa nchini humo mwaka 2011, kabla ya kuanza kampeni ya kumg'oa madarakani
Kanali Muammar Ghaddafi.
Hadi mwaka 2011, Libya ilikuwa inazalishaji mapipa
milioni moja na laki sita kwa siku.


0 comments:
Post a Comment