Waandishi wa habari wameaswa kujiendeleza kielimu
katika fani ya uandishi wa habari na taaluma nyingine ili waweze kukabiliana na
kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.
Wito huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na
Mhadhiri Chuo Kikuu Huria Dr.Hamza Kondo alipokuwa akizindua kitabu chake
kiitwacho Watchdog Journalism in Tanzania a Sustainable Struggle ambapo kwa
Kiswahili ni “Uandishi Habari Huru Tanzania ni mapambano endelevu”.
Dr Kondo amesema lengo la kitabu hicho ni
kuwaelimisha na kuwaasa waandishi wa habari na wataaluma ya habari kuzidi
kuithamini taaluma hiyo licha ya changamoto zinazowakabili.Amesema kitabu hicho
kinazungumzia uhalisia wa uhuru wa habari nchini, hivyo kinafaa kufundishia
taaluma ya habari katika vyuo vikuu na vyuo vya kati nchini.
Aidha,Mhadhiri huyo ameongeza kuwa ili fani ya
taaluma ya habari iheshimike ni lazima iwe na bodi ya wataalamu waliobobea
ambayo itaundwa na wasomi wa taaluma husika ili kusimamia maadili ya taaluma
hiyo na kuchukua hatua kwa wanataaluma watakaokiuka maadili.
Mbali na hayo Dr.Kondo ametoa zawadi ya vitabu kwa
baadhi ya vyombo vya habari nchini likiwemo gazeti la Jamuhuri,gazeti la
majira, gazeti la Habari Leo, gazeti la Mwananchi na gazeti la Nipashe.


0 comments:
Post a Comment