Amesema nchi inatakiwa kuangalia na kujadili
uchaguzi usiwe bidhaa inayotafutwa kwa fedha kama ambavyo ilijitokeza katika
uchaguzi wa mwaka jana ambao rushwa ilitumika kwa kiwango kikubwa.
Akizungumza katika mdahalo wa kitaifa kuhusu
uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana, Warioba pia ametoa angalizo kwa asasi za
kiraia kuwa makini na wafadhili wao kuepuka kuingiza matakwa yao (wafadhili)
kwenye siasa za ndani.
Mdahalo huo uliofanyika jana jijini Dar es Salaam,
ulioandaliwa na Mpango wa Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET) na Kituo cha
Sheria na Haki za Binadamu, (LHRC).
Akiwasilisha mada, Warioba ambaye amepongeza
utendaji wa Rais John Magufuli, alisema uchaguzi mkuu ulikuwa na hamasa ambayo
haijapata kutokea lakini ulikuwa huru na ulimalizika kwa amani na utulivu .
Alisema akiwa mmoja wa waangalizi aliyewahi
kusimamia chaguzi za Zambia, Malawi, Nigeria, Ghana, Ethiopia na Sudan,
anafahamu masuala ya uangalizi na kutoa ripoti. Alisema ni kweli uchaguzi
ulienda vizuri. Alisema alipoangalia maoni ya waangalizi wa nje alishangaa kwa
mara ya kwanza kusifu mchakato mzima wa uchaguzi.
Alisema licha ya kuwapo kwa upungufu mdogo,
waangalizi hao walisifu mchakato mzima na zaidi alishangaa kuona waangalizi
ambao wagumu kusifia ; mfano Umoja wa Ulaya (EU), waliridhishwa na uchaguzi
huo.
Vyama, asasi vyamulikwa
Hata hivyo alisema, katika kukuza demokrasia kwenye
vyama, yapo matatizo na ipo kazi ya kufanya kwa kuwa rushwa imekuwa ikitumika
kwa kuwepo matumizi mabaya ya madaraka.
Alisema bila kuleta demokrasia ndani ya chama, ni
vigumu kufanikiwa katika kukuza demokrasia nchini.
“Ni rahisi kulaumu Tume ya Uchaguzi (NEC) lakini
ndani ya vyama hawafuati yale wanayotaka NEC iwafanyie hivyo lazima kuwe na
demokrasia ndani ya chama kwani kukiwa na vyama bila demokrasia hatupati nchi
yenye demokrasia hivyo wanasiasa tupige kelele ndani ya vyama siyo
NEC,”alisisitiza.
Kwa upande wa asasi za kiraia kuwa walifanya kazi
ipasavyo lakini alishauri elimu kwa mpigakura iwekwe kwenye mtaala wa shule
nchini na isisubiri kutolewa wakati wa uchaguzi.
Asasi na wafadhili
Akizungumzia nafasi ya asasi za kiraia, alisema zipo
baadhi katika kutoa elimu, ziligeuka wanaharakati na kufikia kuhamasisha wachague
chama au mgombea yupi .
Alisema walifanya hivyo ikidaiwa ni matakwa ya
wafadhili jambo alilosema kwamba ni hatari masharti ya wafadhili kuingilia
siasa za nchi.
Wanahabari
Jaji Warioba alizungumzia pia ushiriki wa vyombo vya
habari katika uchaguzi huo na kusema vyote vilikuwa na upendeleo. Alisema hata
magazeti yaliyosifika kwamba hayana upendeleo, yalizidi na mpaka sasa vyombo
hivyo vina upande wake.
Alitaja baadhi ya mambo ya kuboresha ni mfumo wa
kisheria na kitaasisi kwa kuboresha katiba kukuza demokrasia.
Alisema ushindi wa rais uhojiwe mahakamani na kuwepo
kwa kura za uwiano kwa wabunge kuleta usawa wa kijinsia pamoja na vyama vidogo
vya siasa kukua.
NEC kulalamikiwa
Alisema lazima kuwa na tume inayoaminika na wote
ambayo haitawekwa wanasiasa.
Akizungumzia suala la gharama za uchaguzi,Warioba
alisema sheria ipo lakini haitekelezwi kwani vyama vikubwa vinapata faida
kuliko vidogo .
Alisema uchaguzi mkuu wa mwaka jana ulikuwa ni wa
fedha hivyo kugeuka bidhaa kwa wenye fedha kushinda.
Alisema athari zilizojitokeza katika uchaguzi mkuu
ni lugha iliyotumika ya kukebehi ,kukejeli na matusi ikiunganishwa na ushabiki
hali iliyoacha makovu na uhasama katika jamii na miongoni mwa viongozi .
Alisema kumekuwa na nyufa katika taifa kwa kuwepo
rushwa na ubaguzi kwani rushwa imekuwepo katika ngazi zote za mchakato wa
uchaguzi kuanzia uteuzi wa wagombea ndani ya vyama mpaka kutangaza matokeo.
Alisema kumekuwa na ubaguzi wa kila aina ikiwemo
ukabila, dini na kikanda ambao nyuma ulijulikana kijiografia lakini sasa
zinatumika kisiasa .
Alisema zipo nyufa mpya zinazoanza kujitokeza baina
ya wazee na vijana.
Mdahalo huo uliokuwa na kaulimbiu ya ‘Tathmini ya
Uchaguzi Mkuu wa Tanzania mwaka 2015: Mchango wa waangalizi wa ndani kuelekea
uchaguzi bora, huru na haki’, mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria,
Dk Harrison Mwakyembe.
Mwakyembe alisema takwimu za mwaka 2013-2014
zinaonesha kuwa kwa ujumla demokrasia nchini inazidi kuimarika na kushamiri.
Waziri alisema inaonesha kuwa Tanzania ilikuwa nchi
ya 83 ikiwa na alama 50.5 kwa kukidhi vigezo vya demokrasia, ikilinganishwa na
Kenya iliyochukua nafasi ya 93 ikiwa na alama 48.1. Zambia ilichukua nafasi ya
94 alama 48.1; Nigeria nafasi ya 107, alama 40.6 na Afrika ya Kusini ikichukua
nafasi ya 71 alama 54.7.
0 comments:
Post a Comment