Image
Image

Bulaya amfananisha Maghembe na tishu.

MBUNGE wa Bunda Mjini (Chadema), Ester Bulaya amezua mzozo bungeni, baada ya kumwita Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jummane Maghembe kuwa mwepesi kama tishu.
Amemfananisha na tishu (karatasi laini ya kujifutia), kutokana na kile alichodai kushindwa kusimamia mambo mbalimbali, ikiwamo kuirudishia leseni ya uwindaji Kampuni ya Green Miles Safaris Ltd.
Bulaya alitoa kauli hiyo jana bungeni, wakati akichangia hotuba ya makadirio ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Alisema Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, aliwahi kumwita Waziri Mghembe kuwa waziri mzigo, hivyo Maghembe anapaswa kulithibitishia bunge kuwa yeye waziri mzigo kweli, au ni lumbesa (gunia lililojazwa kupita kipimo) au yeye ni mwepesi kama tishu.
“Ule msemo wa Kinana kukuita wewe ni mzigo ni kweli? Au wewe ni lumbesa, au utudhihirishie hapa wewe ni mwepesi kama tishu,” alisema Bulaya.
Baada ya kusema hivyo, ndipo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama, aliposimama na kuomba utaratibu kwa Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge.
Mhagama alisema maneno yaliyosemwa na Bulaya ni ya udhalilishaji na si mazuri ya kumfananisha Waziri na tishu, hivyo anapaswa kutumia maneo mazuri ili ujumbe wake ufike
“Namheshimu sana mdogo wangu Ester, ana uwezo wa kujenga hoja vizuri sana. Lakini nimsaidie kitu asivunje kanuni, bali atumie maneno yanayoweza ku-‘deliver message (kufikisha ujumbe) vizuri,” alisema Mhagama.
Baada ya Mhagama kutoa taarifa hiyo, Chenge alitoa ufafanuzi na kusema tishu ni karatasi nyepesi, lakini kimaudhui ilivyotumika si sahihi. Alisema Maghembe ni waziri wa Tanzania na Bulaya ni mbunge, hivyo anatakiwa kufuta maneno nyepesi.
“Ninakuagiza Bulaya kufuta maneno nyepesi. Mi nakuagiza tu, hebu futa maneno hayo halafu twende mbele,” alisema Chenge.
Bulaya alisimama na kusema alimaanisha wepesi, pia Bulaya alihoji kwa kusema: “Aseme Kinana kumwita mzigo sawa? Sisi tukisema tishu kwa maana ya wepesi siyo sawa? Nimevunja kanuni ipi?”
Baada ya kauli hiyo yaliibuka mabishano kati ya Chenge na Bulaya kama ifuatavyo;-
Chenge: Mheshimiwa unabishana na kiti? Bulaya useme tu kama unakaidi maneno au unafuta.
Bulaya: Biashara ya bunge kutupangia kusema kitu si sahihi.
Chenge : Bulaya keti, nimekuagiza futa neno wepesi, twende mbele.
Bulaya: Nasema hivi kama tishu linakwanza ninamaanisha wepesi. Tishu litoke lakini wepesi libakie pale pale. Atuambie kama yeye ni mzigo au mwepesi.
Hata hivyo, Chenge alikaa kimya na Bulaya kuendelea kuchangia. Alisema Waziri Maghembe anapswa kulieleza bunge hadi sasa ni tembo wangapi wameuwawa kwa ujangili
“Ngorongoro kuna mbuyu pale una ukubwa kama sebule, majangili walitengeneza ndani ya hifadhi ya Tarangire, nataka kujua wizara yako imepoteza tembo wangapi? Ukinijibu hayo nitajua wewe ni mwepesi au mzigo,” alisema Bulaya.
Kadhalika, Bulaya alihoji hatua ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuirudishia leseni ya uwindaji Kampuni ya Green Miles Safaris Ltd wakati mwaka jana kampuni hiyo ilinyang’anywa leseni na Waziri aliyetangulia.
“Ni sababu zipi wizara hiyo hiyo moja inatofautiana kauli, kwenye hiyo kampuni, kuna kitu gani? Nini kimezunguka? Huyo mtu anachezea sharubu za serikali. Haiwezekani wizara hiyo hiyo inakuwa na kauli mbili zinazopingana, au hamuiamini tume ya wanyamapori,” alisema.
MSIGWA ACHARUKA
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa, ameitaka serikali kutekeleza maazimio ya Bunge la Kumi, likiwamo la utekelezaji wa hatua zitakazobainisha waliohusika katika tukio la kutorosha wanyama hai chinini, kuwapeleka nje ya nchi kuchukuliwa hatua.
Msigwa ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Maliasili na Utalii, aliyasema hayo jana wakati akichangia hotuba ya wizara hiyo na kusema kuwa maazimio hayo hayapaswi kuendelea kuwa viporo.
“Kama tunataka kukomesha ujangili, turejee kwenye hatua zilizokuwa zimefikiwa kabla ya serikali hii kuingia madarakani, ambazo zilikwama au kukwamishwa na mambo mbalimbali na kwasababu serikali hii imejipambanua kwa kufukua ‘makaburi’ basi tuanze kufukua kaburi hilila vita dhidi ya majangili,” alisema Msigwa.
Kadhalika, Msigwa alimtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, kutoa msaada kwa bunge ili kutekeleza maazimio hayo likiwemo la kurejesha wanyama waliotoroshewa Qatar kwa kuwa naye alikuwapo katika bunge lililopita lililofanya maazimio hayo.
Msigwa alisema yeye (Msigwa) alikuwa miongoni mwa kamati yenye wabunge wanne waliokuwa wanachunguza utoroshwaji wa wanyama na kubaini kuwa kampuni ya Green Miles Safaris Ltd haikupewa vitalu vya uwindaji kutokana na kukosa sifa.
Alisema Kamati ya Ushauri ilimshauri waziri kuwa kampuni hiyo ilikosa sifa kwa sababu haina uwezo wa kuhifadhi lakini kwa bahati mbaya, kampuni hiyo ikapewa kibali cha kuwinda kabla dunia haijashuhudia majanga yalitokana na uvunjwaji wa kanuni za uwindaji.
Alisema kampuni hiyo iliwinda Ngedere, huku watoto chini ya miaka 16 walishuhudiwa wakifanya uwindaji, wakati sheria inazuia matumizi ya bunduki zinazozuia milio lakini kampuni hiyo walikuwa wakitumia silaha nzito.
    Share on Google Plus

    Kuhusu TAMBARARE HALISI

    This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

    0 comments:

    Post a Comment