Image
Image

Kesi ya tumbili wekundu 61 kuibua mazito.

KESI ya kusafirisha tumbili wekundu 61 kwenda ughaibuni, inayomkabili Mkurugenzi Msaidizi wa Wanyamapori, Dk. Charles Mulokozi na wenzake sita, imeanza kuibua mazito, baada ya mawakili wa utetezi, kuhoji Mahakamani nia ya serikali kuchelewesha uchunguzi.
Wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ya uhujumu uchumi, namba 1 ya mwaka 2016, ni Nyangabo Musika, Martina Nyakangara, Very Gerald Anthony (wote maofisa wa Wizara ya Maliasili na Utalii), Iddy Misanya (mfanyabiashara), Artem Verdanian na Eduard Verdanian, (wote raia wa Uholanzi).
Wakili Robert Rogath, akiwa mbele ya Joachim Tiganga, ambaye ni Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi-Moshi, alihoji kuchelewa kukamilika kwa uchunguzi huo, wakati vielelezo vya ushahidi pamoja na washtakiwa vilikamatwa papo hapo, katika eneo la tukio.
Hoja ya mawakili hao, iliibuka baada ya Wakili wa Serikali, Lucy Kyusa, kudai mahakamani hapo kwamba upelelezi wa shauri hilo, bado haujakamilika.
Baada ya hoja hiyo, Hakimu Tiganga aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 27, mwaka huu, itakapotajwa tena na kutoa amri kwa washtakiwa kurejeshwa rumande.
Tumbili hao wenye thamani ya Dola za Marekani 7,320 sawa na Sh. milioni 15.8 za Tanzania, walikamatwa Machi 23, mwaka huu, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), wakitaka kusafirishwa kwenda Armenia, Ulaya Mashariki.
Katika kosa la kwanza, washtakiwa wote kwa pamoja, wanadaiwa katika eneo lisilojulikana kati ya Machi Mosi na Machi 22, mwaka huu katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Dar es Salaam, walihusika kula njama ya kutenda kosa hilo la utoroshaji wa nyara za serikali.
Kosa la pili ni la kujihusisha kutenda kosa la uhujumu uchumi, kinyume cha aya 4 (1) (d) cha maudhui ya Kifungu cha 57 (1), na 60 (2) cha Sheria ya Udhibiti wa Uhujumu Uchumi, Sura ya 200 ya Sheria iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.
Kosa la tatu, wanadaiwa kujihusisha na utoroshaji wa nyara za serikali, kinyume cha Kifungu cha 80 (1), 82 (1) na 84 (1) cha Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009, ikisomeka sambamba na aya ya 14 (b) ya maudhui ya kifungu cha 57 (1) na 60 (2), cha sheria ya kupambana na makosa ya uhujumu uchumi, Sura ya 200 ya Sheria iliyofanyiwa Marejeo mwaka 2002.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment