Image
Image

Huhitaji uchawi kumjua mchawi wa kwanza Simba.

NDANI ya dakika 90 za soka la Tanzania kuna mengi. Naamini kuna watu wanakesha wakiroga, naamini kuna watu wanakesha wakitafuta hoteli walizofikia waamuzi, naamini kuna watu wanakesha wakitafuta namba za simu za wachezaji wa timu pinzani. Niweke wazi kwamba naamini hayo.

Utakuwa ni uongo na ujinga kutoamini hayo. Yapo katika soka la Tanzania. Kama mtu kama Abdalah Kibadeni anasema yapo, nani wa kumbishia? Sijui kwa nini hakuwahi kuitwa kutoa ushahidi. Kama Zacharia Hans Poppe amewahi kukaririwa akisema haya yapo, mimi ni nani nipinge.

Hata Evans Aveva, Rais wa Simba alipotuna katika meza za hoteli ya Colosseum akitoa sababu za Simba kukosa ubingwa msimu huu, hakunishangaza sana alipotaja hayo hapo. Ni sehemu ya soka la Afrika, lakini zaidi ni sehemu ya soka la Tanzania.

Bahati mbaya, juu ya kila kitu, Aveva alishindwa kuweka bayana mchawi wa Simba.

Mchawi mkubwa wa Simba ni mabadiliko makubwa yaliyoingia katika mchezo wa soka ambayo si tu yanaisumbua Simba, lakini yanasumbua hata soka la Ulaya kwa sasa. Mpira pesa!

Kila fitina ya soka katika zama hizi inasaidiwa kwa kiasi kikubwa na ubora wa kikosi chako uwanjani. Ndiyo maana naamini, bila ya Yusuf Manji, kwa pesa ambazo Azam imetumbukiza katika kikosi chao ingeweza kuwa mabingwa kwa miaka hata minne mfululizo. Bila ya pesa za familia ya Bakhressa ni wazi kwamba Yanga nayo ingeweza kuwa bingwa kwa zaidi ya misimu minne mfululizo.

Kinachotokea kwa timu kama Azam ni kile kile ambacho pesa za Roman Abramovich kimepeleka katika Ligi Kuu ya England tangu mwaka 2003. Ni kama ilivyo pia kwa Man City, na ni kama pia ilivyo kwa PSG. Dunia inaathirika na mfumo mpya wa matumizi makubwa ya pesa.

Simba hii hii ingeweza kuwa bingwa kama Yanga isingekuwa na Manji au Azam isingeanzishwa. Naamini hivyo. Wala watu wasingeona ubovu wa Simba hii. Nani alijua kuwa Arsenal na Manchester United zilikuwa na mapungufu mengi mpaka alipokuja Roman Abramovich na pesa zake? Kwa mfano, Simba imechukua wachezaji wawili waliocheza Azam miaka ya karibuni, Joseph Kimwaga na Brian Majwega. Inakuaje Simba wanachukua wachezaji walioachwa na Azam? Unategemea wachezaji wanaocheza katika nafasi zao pale Azam watakuwa na ubora gani? Leo Simba ni timu ya kutegemea wachezaji walioachwa Azam? Unapataje matokeo?

Achana na Hamis Kiiza aliyejitahidi sana msimu huu, hivi ni kweli Dan Lyanga anaweza kuwekwa katika mizani moja na Donald Ngoma au Kipre Tchetche? Wakati Lyanga akiwa na namba yake Simba, Didier Kavumbagu hana nafasi ya kudumu katika kikosi cha Azam. Paul Nonga na Malimi Busungu hawana nafasi za kudumu Yanga.

Hata hivyo, Dan amepatikana kwa bei yake, huku hawa kina Ngoma na Kavumbagu wakipatikana kwa bei zao. Wana bei tofauti na wanaleta matokeo tofauti.

Maisha haya yapo Ulaya kwa sasa. Ukilitazama benchi la Man City au PSG unakuta wachezaji ambao wanaweza kuanza katika kikosi cha kwanza cha Arsenal au Manchester United. Ni wazi kwamba unahitaji pesa nyingi kabla ya kuingia katika mapambano ya soka la siku hizi.

Matukio mengi ambayo yamesababisha watu kusema Yanga inabebwa yametokana na ukali wa mashambulizi yao ya mara kwa mara. Wanafika sana langoni mwa adui. Ndiyo maana unapokosoa kubebwa kwa Yanga utajikita zaidi katika kadi nyekundu za mabeki wa timu pinzani, kama ile ya Banda, bao linalosemwa kuwa la mkono la Amiss Tambwe dhidi ya Coastal Union, bao linalosemwa lakuotea la Ngoma dhidi ya Coastal Union. Ni dalili ya timu nzuri inayoshambulia.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment