MKUU
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametoa siku 90 kwa viwanda
vinavyozalisha mifuko ya plastiki, kutozalisha mifuko hiyo kwa kuwa
imekuwa ikichangia katika uchafuzi wa mazingira. Pia amewataka
wazalishaji wa mifuko hiyo, kuiga mfano wa Zanzibar, ambayo imefanikiwa
kudhibiti matumizi ya mifuko hiyo.
Alitoa agizo hilo jana wakati
akizindua kampeni ya usafi ya siku 90 yenye lengo la kuhakikisha mkoa
huo unakuwa na mazingira safi ambayo itahusisha mashindano ya mitaa ya
jiji, iliyopangwa na isiyopangwa.
Hatua hiyo imefikiwa kutokana na
agizo la Rais John Magufuli alilotoa Desemba mwaka 2015, ambapo katika
utekelezaji wake, Makonda amebuni shindano hilo ambalo mshindi atapata
Sh milioni 50.
“Naomba muige watu wa Zanzibar, wana mifuko lakini si
ya plastiki. Ndani ya siku 90 kuanzia leo (jana) sitaki kuona mifuko ya
plastiki ndani ya mkoa wangu... Tuachane na hii mifuko ambayo kwanza
kimsingi ni ngumu kuiteketeza, lakini hata ukiamua kuiteketeza madhara
yake ni makubwa,” alisema Makonda.
Katika hatua nyingine, Makonda
amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa (RAS), Theresia Mmbando, kuanzia kesho
aunde kamati ya uchunguzi wa kampuni za usafi zinazomilikiwa na
watumishi wa umma, ili ziondolewe kwa kuwa ni kinyume cha maadili ya
utumishi wa umma.
Alisema katika mkoa huo kuna watumishi wameanzisha
kampuni za kusafisha miji, lakini kwa mujibu wa maadili ya utumishi wa
umma kipengele cha mgongano wa maslahi hakiruhusu watumishi kumiliki
kampuni za kutoa huduma hizo kwa jamii.
“Pia naagiza waende
kuangalia, kampuni nyingi zinazopewa zabuni hazina vifaa kama
zilivyoeleza kwenye makaratasi yao, wamejieleza kuwa na magari saba,
wafanyakazi 100 na mifagio lakini ukienda wanapofanya usafi hakuna
kitu,” alisema.
Alisema mkoa huo hutumia zaidi ya Sh bilioni sita kwa
mwaka kukusanya uchafu, lakini bado jiji linakuwa chafu na kutaka fedha
hizo ziendane na matokeo ya usafi uliokusudiwa. Aidha aliwaasa vijana
kufanya kazi ili kuleta maendeleo kwani Rais Magufuli anawaamini vijana
na kuonesha kuwa wamelelewa vizuri na kufundishwa uadilifu na kupewa
moyo wa kujituma na kufanya kazi.
“Usikubali kumuona mtu anachafua
mazingira na wewe ukiwepo. Lakini matrafiki wote kuanzia Jumatatu, nataka mkague daladala kama wameweka chombo cha taka ndani ya
magari yao,” alisema.
Pia aliwataka makondakta kuhamasisha watu kuwa
wasafi kwa kuelekeza abiria sehemu ya kutupa taka wawapo ndani ya
daladala. Naye Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi, alimuagiza
Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, kutoa taarifa za hatua alizowachukulia
maofisa watatu wa wilaya hiyo walioshindwa kutekeleza majukumu yao
katika kufanikisha kampeni hiyo.
“Ifikapo Jumanne mchana, niwe
nimepata taarifa za hatua za kinidhamu walizochukuliwa watumishi hawa
ambao ni Abiyu Peter, Ofisa Usafishaji, Ofisa Utumishi, Josia Kiverenge
na Ofisa Utamaduni, Joyce Kirio,” alisema.
Home
News
Slider
Makonda atoa siku 90 kwa viwanda vinavyozalisha mifuko ya plastiki kutozalisha mifuko hiyo.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment