WATOTO
kati ya 100 hadi 150 kila mwaka nchini hufikishwa katika Hospitali ya
Taifa Muhimbili (MNH) ili kupatiwa matibabu dhidi ya ugonjwa wa saratani
ya jicho.
Takwimu hizo zilitolewa jana Dar es Salaam na Dk. Anna Sanyiwa wa MNH Kitengo cha Saratani wakati Alipokuwa akizungumzia suala hili juu ya maadhimisho ya wiki ya kimataifa ya kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu saratani ya jicho kwa watoto.
“Maadhimisho
haya hufanyika kuanzia Mei 8 hadi 15 kila mwaka yakiwa na lengo la
kupeleka elimu kwa jamii juu ya ugonjwa huu. Hapa Muhimbili tumekuwa
tukipokea watoto kati ya 100 hadi 150 kila mwaka wenye tatizo hili
ambalo kitaalamu linajulikana kama ‘Retinoblastoma,” alisema.
Alifafanua
kuwa saratani hiyo hutokana na hitilafu inayotokea kwenye vinasaba
(genetic defect) ambayo huathiri katika utando wa fahamu wa jicho, na
kwamba huanza kujitokeza baada ya miaka mitatu ya uhai wa mtoto tangu
alipozaliwa.
“Hata hivyo mara chache sana hujitokeza baada ya miaka
mitano. Saratani hii huwapata watoto wa jinsi zote kwani inahusisha
vinasaba, yaani inarithiwa. Kuna uwezekano wa asilimia 50 ya familia
yenye vinasaba hivi kupata mtoto mwenye ugonjwa huu.
“Takwimu
zinaonyesha pia asilimia 60 ya watoto wanaorithi vinasaba hivyo hupoteza
macho yao yote mawili, lakini asilimia 40 huathirika jicho moja, hasa
wale ambao wazazi wao huwa wameoana huku wakiwa ni ndugu wa karibu,”
alisema.
Alisema kwa kipindi cha miaka mitatu hadi minne iliyopita, wamekuwa wakipokea idadi kubwa ya wagonjwa kutoka Kanda ya Ziwa.
“Takwimu
zetu zinaonyesha hivyo, lakini bado tunaendelea kuzichambua na hata
kuangalia kwanini wengi wanatokea katika kanda hiyo kuliko kanda
nyingine hapa nchini,” alisema.
Dk. Sanyiwa alisema mara nyingi
dalili za ugonjwa huo huwa zinafanana kwa karibu na dalili za magonjwa
mengine ya macho, na kwamba daktari bingwa wa macho ndiye anaweza
kuangalia na kutofautisha saratani na magonjwa mengine.
“Dalili
zenyewe hutegemea hatua ya ugonjwa, hata hivyo dalili za mwanzo huwa ni
jicho kuonyesha weupe kwenye mboni, mtoto wa jicho, jicho kuwaka kama
paka usiku au mwanga mweupe ukipiga picha na ‘flash’,” alisema.
Alitaja dalili nyingine kuwa ni kengeza, weupe kwenye kioo cha jicho, jicho kuvilia damu, kuwa jekundu na kuuma.
“Dalili nyingine hutokea ugonjwa unapoendelea kukomaa kwa mfano hufika mahali hadi jicho linakuwa kubwa na kuvimba,” alisema.
Daktari huyo aliwashauri wazazi kuwafikisha watoto mapema hospitali pindi wanapoona dalili za aina hiyo.
“Mbali
na Hospitali ya Taifa Muhimbili, bado kuna vitengo vingine vya macho
katika Hospitali ya Rufaa ya Kilimanjaro Christian Medical Centre (KCMC)
pamoja na Bugando, Mwanza,” alisema.
Home
Afya
Slider
Saratani ya jicho inahatarisha maisha kwa watoto zaidi ya 100 kila Mwaka nchini Tanzania.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment