HATIMAYE
wakazi wa Dar es Salaam wamepata nyenzo mpya ya usafiri ndani ya jiji
hilo, baada ya kusubiri kwa muda mrefu kukamilika kwa mradi wa mabasi
yaendayo haraka wa Kampuni ya UDA-RT na kuanza rasmi majaribio ya
kusafirisha wakazi wake.
Tunapenda kuwapongeza wadau wote
walioshiriki kufanikisha mradi huu hadi kufikia hatua hii ya uhalisia wa
kuanza kazi. Hakuna ubishi kwamba mradi huu ni faraja kubwa kwa wakazi
wa Dar es Salaam kutokana na ukweli kwamba kwa muda mrefu, wamekuwa
wakikabiliana na msongamano na foleni kubwa ya vyombo vya usafiri wakati
wa kwenda na kurudi katika shughuli zao mbalimbali jijini.
Kuna kila
aina ya matumaini kwamba kupatikana kwa usafiri wa DART, kutupunguza
kwa kiasi kikubwa kero ya usafiri, msongamano na foleni kwa wakazi wa
jiji na hivyo kuwarahisishia kufika kwa wakati katika maeneo yao
mbalimbali ya kazi na shughuli nyingine za kijamii.
Miundombinu ya
barabara za DART na mabasi yenyewe ni ya kisasa, kiasi kwamba abiria
wanahitaji kujifunza masuala muhimu na ya msingi katika kupata huduma
hiyo kwa urahisi na kwa uhakika zaidi.
Hapa tunapenda kumuunga mkono
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa kuongeza muda wa kutoa
elimu kwa abiria wa mabasi hayo hadi Jumapili, kwa abiria kupanda bure
kwa lengo la kujifunza.
Awali muda huo wa mafunzo kwa abiria ulikuwa
ni siku mbili na ungemalizika jana. Tunapenda kutoa wito kwa abiria,
watembea kwa miguu na watumiaji wengine wa vyombo vya usafiri ikiwa ni
pamoja na magari madogo, bajaji, bodaboda, guta na baiskeli kuheshimu
sheria za barabarani na pia kutoingilia barabara ya mabasi ya mwendo wa
haraka ili yaweze kufanya kazi zake kwa ufanisi kama ilivyokusudiwa.
Tayari
viongozi wetu mbalimbali wakiwemo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda na Kamanda wa Kikosi cha Usalama
Barabarani, Mohamed Mpinga wameshalisemea suala la vyombo vingine vya
usafiri kuheshimu sheria za barabarani na kwamba barabara ya mabasi
yaendayo kasi ni kwa ajili ya mabasi hayo tu.
Katika hili tunawaomba
wananchi pamoja na watumiaji wa vyombo vingine vya usafiri, wajifunze na
kuheshimu barabara hizo ili nia njema ya mradi huo wa DART isivurugwe
na wachache, wasiotaka kufuata sheria za usalama barabarani na
kutufikisha kwenye mikasa ya ajali kwa uzembe wao wa makusudi wa
kutofuata sheria.
Katika hili tunaomba wananchi wote na wenye vyombo
vingine vya usafiri, tubadilike kwa kujifunza utamaduni wa kutii sheria
bila shuruti ili tuweze kufurahia huduma hiyo mpya na ya kisasa ya
usafiri wa mabasi ya haraka.
Tunapenda pia kusisitiza kwamba vyombo
vyenye dhamana ya usalama barabarani, hususan Kikosi cha Usalama
Barabarani chini ya uongozi wa Mpinga, wawachukulie hatua zinazostahili
wote watakaokuwa wanakiuka utaratibu wa kuheshimu sheria za usalama
barabarani, ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani kupata adhabu
wanayostahili bila kufanya ajizi.
Lakini, hatua pia zichukuliwe dhidi
ya wale watakaojaribu kuharibu miundombinu ya DART na mabasi yake.
Katika hili, wananchi wote kwa ujumla wao, kila mmoja awe mlinzi wa mali
hizo kwa kuripoti katika vyombo husika, watakaojaribu kuharibu
miundombinu hiyo muhimu.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment