KATIKA
kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana, Rais John Magufuli na Makamu wa
Rais, Samia Suluhu Hassan, waliwaahidi wananchi kuwa Serikali ya Awamu
ya Tano, itawatumikia na kujali wananchi wote, hasa wananchi wa kawaida.
Pia,
waliahidi kuwa kazi na mipango yote itakayopangwa na kusimamiwa na
serikali, itatatua kero mbalimbali za wananchi, itaongoza mabadiliko
makubwa ya kiutendaji, kusimamia matumizi ya mali za umma na rasilimali
za taifa, na kugawa rasilimali hizo kwa haki.
Rais amekuwa
akisisitiza kuwa mambo waliyoyaahidi kwa wananchi, watayatekeleza kwa
sababu ahadi ni deni ; na kwamba wananchi wawaamini kuwa hawakutoa ahadi
hizo ili tu wawapigie kura, bali kwamba hicho ndicho serikali
inachofanya.
Ni dhahiri wananchi wamedhihirisha ukweli wa maneno hayo
ya Rais Magufuli, hasa waliposikiliza hotuba yake ya Sherehe za Mei
Mosi, zilizofanyika kitaifa mkoani Dodoma.
Katika hotuba hiyo Rais,
alifafanua hatua mbalimbali ambazo serikali yake imechukua tayari ; na
zile itakayozichukua kuanzia mwaka ujao, kuboresha maisha ya wananchi,
wakiwemo wafanyakazi wa kawaida.
Kwa mfano, hatua mojawapo ni
kupunguza kodi inayokusanywa na serikali katika mishahara, maarufu kama
Pay as You Earn (PAYE) kutoka asilimia 11 hadi asilimia 9 kuanzia mwaka
ujao wa fedha wa 2016/17.
Anasema kwa muda mrefu, wafanyakazi
wamekuwa wakiomba serikali ipunguze PAYE ; na kwamba sasa serikali
imesikia kilio hicho. Hatua hiyo itawapunguzia makato wafanyakazi hao na
kuwapa ahueni kubwa.
Kiwango hicho cha PAYE kitakapopunguzwa,
kutakuwepo na pengo katika makusanyo ya kodi za serikali, lakini tuna
imani serikali hiyo hiyo, itapanua vyanzo vyake vya kodi, kufidia pengo
hilo.
Jambo lingine ambalo Rais Magufuli amewaahidi wafanyakazi ni
kuwa hapo baadaye serikali itapandisha mishahara, lakini kwamba serikali
imeona ianze kwanza na suala hilo la PAYE, ambalo limekuwa
likilalamikiwa kwa muda mrefu na watumishi.
Hatua nyingine Rais
alibainisha kuwa itawanufaisha watu wa kawaida ni kuendeleza msako wa
watumishi hewa ili fedha zitakazookolewa, zitumike kuboresha mishahara.
Wapo watumishi wengi wanaofanya kazi kwa bidii na uaminifu wa hali ya
juu. Lakini, wapo wachache ambao ni wafanyakazi hewa, ambao wamekuwa
wakilipwa mishahara bila kufanya kazi.
Baadhi ya watu hao ama walishakufa, walishafungwa, walishastaafu au wapo masomoni.
Msako
wa wafanyakazi hewa unaondelea nchini, umebaini kuwa hadi jana kulikuwa
na wafanyakazi hewa 10,295, ambapo 8,000 ni kutoka Serikali za Mitaa na
karibu 2,000 wa Serikali Kuu ambao wamekuwa wakilipwa jumla ya Sh
bilioni 11 kwa mwezi na kwa mwaka karibu Sh bilioni 139 na kwa miaka
mitano Sh bilioni 996.
Ni wazi fedha ambazo zinatumika kulipa
watumishi hewa kwa miaka mitano; zinatosha kabisa kujenga daraja la
kisasa, kama Daraja la Nyerere, Kigamboni Dar es Salaam lililofunguliwa
juzi; au zingeweza kujenga hospitali nyingi na shule nyingi za kisasa.
Kwa
hiyo, kinachotakiwa kufanywa kwa sasa ni tuendelee kuwafichua
wafanyakazi hewa ; na pia turipoti kwa vyombo vya dola maofisa wote wa
serikali, wanaoendelea kuwalipa ili serikali iwachukulie hatua kali.
Jambo
la pili ni wafanyazi wote tuiunge mkono Serikali ya Rais Magufuli, kwa
kujituma na kuchapa kazi kwa bidii, weledi na uaminifu wa hali ya juu.
Mungu Ibariki Afrika. Mungu Ibariki Tanzania.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment