Wapiganaji wa kiarabu na Kikurdi wakisaidiwa na wanajeshi wa Marekani wamekabiliana na kundi la Dola la Kiislamu katika ngome yao mjini Raqa nchini Syria huku vikosi vya Iraq vikikaribia kuukomboa mji wa Fallujah, Iraq.
Operesheni hizo mbili dhidi ya Dola la Kiislamu zimeelezwa kuwa muhimu katika kuwavunja nguvu wanamgambo wa kundi hilo tangu lilipotangaza utawala wa kiislamu nchini Iraq na Syria mwaka 2014. Karibu na uwanja wa mapambano kaskazini mwa mji wa Raqa, mpigaji picha wa shirika la habari la AFP aliwaona wanajeshi wa Marekani wakiusaidia muungano wa Wakurdi na Waarabu unaojulikana kama Syrian Democratic Forces, SDF.
Muungano huo unapita katika vijiji na maeneo ya mashamba kusini mwa mji wa Ain Issa, kilometa 60 hivi kutoka Raqqa na umevikomboa vijiji vitano na mashamba manne.
Shirika linalofuatilia masuala ya haki za binadamu nchini Syria limesema leo kwamba muungano unaoongozwa na Marekani umefanya mashambulizi yasiyopungua 150 dhidi ya wapiganaji wa Dola la Kiislamu katika miji ya Tal Abyad na Ain Issa tangu operesheni ilipoanza Jumanne wiki hii. Shirika hilo pia limesema wapiganaji wapatao 31 wa dola la kiislamu wameuliwa katika makabiliano kaskazini mwa mkoa wa Raqa.
Hakuna terehe ya kufanyika mazungumzo
Huku haya yakiarifiwa, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mzozo wa Syria Staffan de Mistura alisema mazungumzo kuhusu mzozo huo hayatafanyika katika wiki zijazo. De Mistura amelifahamisha baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu azma yake ya kuanza duru nyingine ya mazungumzo haraka iwezekanavyo, lakini si katika wiki mbili au tatu zijazo.
Mjumbe huyo alielezea kuvunjwa moyo na ugumu uliopo katika kutoa huduma za kibinadamu Syria, hatari kubwa inayoukabili mkataba wa kusitisha uhasama, na haja ya kuhakikisha mazungumzo ya kisiasa yanapiga hatua.
De Mistura ataendelea kuwasiliana na pande zinazohasimiana pamoja na kushauriana na kundi la kimataifa linalosaidia juhudi za kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa Syria, mpaka atakapokuwa katika nafasi ya kuamua juu ya wakati muafaka wa kuanza mazungumzo.
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Samantha Power, alisema Marekani ina wasiwasi kuhusu hali ya kukata tamaa nchini Syria. Power alidokeza kwamba machafuko yameongezeka katika mwezi uliopita na ni dhahiri kitisho kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kinasababishwa na utawala wa Syria na washirika wake, na mashambulizi dhidi ya raia.
"Urusi ina jukumu maalumu kuushinikiza utawala wa Syria kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano na kukomesha mashambulizi ya mabomu na kuwazingira raia wa Syria wasio na hatia," aliongeza Power.
Kaburi la pamoja lagunduliwa
Wakati huo huo, shirika la haki za binadamu la Syria limesema kaburi la pamoja lenye maiti kiasi 65 za watu waliouliwa na wanamgambo wa dola la kiislamu limegunduliwa na vikosi vya serikali karibu na uwanja wa ndege wa jeshi katika mji mkongwe wa Palmyra.
Shirika hilo limesema maiti hizo ni za wanachama wa vikosi vya serikali na nchi washirika walioonyongwa baada ya kundi la Dola la Kiislamu kuuteka na kuudhibiti mji wa Palmyra Mei 2015. Serikali ya Syria mjini Damascus haijathibitisha taarifa hizo.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment