WATU watano wamefariki dunia papo hapo na wengine 26 kujeruhiwa
kutokana na basi mali ya Kampuni ya NBS walilokuwa wakisafiri kutoka Dar
es Salaam kwenda Tabora kupinduka wilayani Gairo mkoa wa Morogoro.
Basi hilo lenye namba za usajili T909 BXK aina ya Yutong, lilipata
ajali saa 5.20 asubuhi katika kijiji cha Tabu Hoteli, kata ya Chakwale,
wilaya ya Gairo katika barabara kuu ya Morogoro- Dodoma.
Miongoni mwa waliofariki kutokana na ajali hiyo ni watu wazima
watatu, wakiwamo wanawake wawili na wanaume watatu ambao pia wamo watoto
wadogo wawili. Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonce
Rwegasira alithibitisha ajali hiyo na kueleza kuwa basi hilo lilikuwa
katika mwendo kasi na liliacha njia ya kupinduka.
Aliitaja baadhi ya miili iliyotambuliwa ni Salmin Shaaban mtoto
mwenye umri wa miezi sita, mkazi wa Urambo na Clement Mpondi umri wa
miaka 40 hadi 50. Kaimu Kamanda Rwegasira alitaja miili ambayo
haijatambuliwa ni ya wanawake wawili mmoja anayekadiriwa kufikia umri wa
miaka 60-65 na mwingine umri kati ya miaka 20-25.
Alisema mwanamke huyo mwenye umri unaokadiriwa kuwa wa miaka 20-25,
alikutwa akiwa amemkumbatia mwanawe wa kiume anayekadiriwa kuwa na umri
wa miezi minne hadi tisa, pia alifariki dunia.
Alisema kati ya majeruhi hao, saba hali zao zilikuwa mbaya na
walipekekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya
matibabu zaidi na wengine walitibiwa na kuruhusiwa.
Alisema majeruhi waliotibiwa na kuruhusiwa na abiria wengine walikuwa
wakifanyiwa mipango na kampuni hiyo kupata usafiri mwingine kwa ajili
ya kuendelea na safari yao kwenda Tabora.
Pia alisema maiti waliotambuliwa na wasiotambuliwa, wamehifadhiwa
katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Morogoro kwa ajili ya kusubiri ndugu kutambuliwa na wengine kuchukuliwa.
Pamoja na hayo, alisema idadi kamili ya abiria waliokuwamo katika
basi hilo haikujulikana kutokana na fomu ya orodha ya majina ya abiria
waliokuwa wamekatiwa tiketi kutoonekana, huku dereva na kondakta wake
wakitoweka eneo hilo na kutokomea kusikojulikana.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment