Image
Image

Mapori yaliyo kwenye Makazi ya watu yatumika kuwa Maficho ya wahalifu Dar.

MAPORI yaliyo kwenye makazi ya watu katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam yametajwa kutumiwa kama maficho ya wahalifu wakiwemo majambazi. Serikali imeombwa kuingilia kati watu wanaohodhi maeneo hayo yaliyotelekezwa na kugeuka mapori, ama wayafanyie usafi wa mara kwa mara au wayapime yagawiwe kwa watu wengine wajenge nyumba.
Ombi hilo kutoka kwa wakazi wa maeneo mbalimbali yaliyo nje ya jiji, limekuja huku kukiripotiwa kuwapo wimbi la ujambazi kutokana na mfululizo wa uvamizi katika makazi na biashara unaoambatana na kujeruhi, kuua na kuiba mali.
Miongoni mwa maeneo yaliyotajwa kukumbwa na mapori yaliyogeuka maficho ya wahalifu ni pamoja na Kibamba, Mbezi, Mbweni na Tegeta wilayani Kinondoni. Mengine ni Kigamboni wilayani Temeke.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi wa maeneo hayo, walisema baadhi ya watu waliokumbwa na uvamizi wa majambazi, ni wanaoishi karibu na maeneo yenye msitu. “Huu msitu ndiyo unatukwamisha.
Hata ukisema ulinzi shirikishi, inakuwa vigumu kwa sababu baada ya kuvamia nyumba, wanakimbilia kwenye huu msitu,” alisema mmoja wa wakazi wa eneo la Muongoni katika kata ya Kibamba.
Hivi karibuni, akizungumza kwenye msiba uliotokea Kibada, Kigamboni ambako Anathe Msuya aliuawa kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Nyakwale Kibada, Said Pazi alikiri mapori kuwa hatari kwa usalama.
Alihimiza wenye viwanja ambavyo havijajengwa wavifanyie usafi kuondoa vichaka ambavyo ni hatari kwa usalama wa raia. Aidha, katika mkutano wa Serikali ya Mtaa wa Kibwegere, kata ya Kibamba uliofanyika hivi karibuni kujadili suala la ulinzi, baadhi ya wakazi walilalamikia mapori na kusema yanakwamisha harakati za ulinzi na udhibiti wa majambazi.
Wananchi hasa wa mtaa wa Kibwegere, waliomba uongozi wa kata usaidie kuhakikisha mapori hayo yanaondolewa baada ya nyumba takribani nne zilizo karibu na pori, kuvamiwa kwa mpigo na kuporwa na wakati huohuo mtu mmoja kuuawa.
Walipozungumzia wimbi hilo la ujambazi hivi karibuni, makamanda wa Polisi katika mikoa ya kipolisi ya mkoani hapa walihakikishia umma kuwa hatua za makusudi zinafanyika ikiwa ni pamoja na kubaini mtandao wa uhalifu.
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kinondoni, Christopher Fuime, alithibitisha kuwepo kwa matukio ya ujambazi katika maeneo mbalimbali ambayo hata hivyo alisisitiza kuwa hatua zinachukuliwa kuyadhibiti.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment