Hukumu hiyo ilisomwa jana mahakamani hapo kwa zaidi ya saa tatu mbele ya Jaji Paul Kihwelo.
Mwangosi aliuawa Septemba 2, 2012 katika eneo la Nyololo wilayani Mufindi mkoani hapa, baada ya askari kuzuia mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Upande wa Jamhuri uliwasilisha mahakamani mashahidi wanne ambako ushahidi wa shahidi wa kwanza, wa pili na wane, wote kwa pamoja ulishindwa kutoa vielelezo vya wazi dhidi ya mshtakiwa huyo kuwa aliuwa kwa kukusudia.
Jaji Kihwelo alisema jukumu la kuonyesha mshtakiwa alitenda kosa hilo ama la, lilikuwa la upande wa Jamhuri ambao walipaswa kuwasilisha ushahidi ambao ungeweza kumtia hatiani mshtakiwa pasi na kuacha shaka ya aina yoyote.
Alisema mahakama inajiuliza juu ya ushahidi uliowasilishwa na shahidi namba moja, mbili na nne.
Jaji alisema shahidi namba tatu ambaye ni Mlinzi wa Amani, Flora Mwolera ndiye aliyetoa ushahidi unaoweza kutumiwa na mahakama kufikia uamuzi.
Kwa mujibu wa ushahidi wa Flora ni kwamba mtuhumiwa alikiri kumuua Mwangosi bila kukusudia na mahakama ilijiridhisha na ushahidi huo pasi na shaka yoyote hivyo ilimtia hatiani mshtakiwa kwa kosa hilo.
Alisema upande wa utetezi kupitia shahidi namba moja ambaye ni mtuhumiwa, kukana ungamo hilo kuwa alilitoa kwa mlinzi wa amani akiwa hayuko huru mahakamani, ilipingana na maelezo hayo kwa kuwa yangepaswa kupingwa kabla kesi haijafungwa.
“Lilikuwa ni jukumu la upande wa utetezi kuleta pingamizi la kukataa ungamo hilo kabla ya kesi kufungwa kwa njia ya maandishi ama ya mdomo hivyo utetezi huo hauwezi kuzuia mahakama kumtia mtuhumiwa hatiani.
“Upande wa Jamhuri umeshidwa kuleta ushahidi unaojitosheleza bila ya kuacha shaka kuwa mtuhumiwa alimuua Mwangosi kwa kukusudia.
“Hivyo mahakama itatumia ushahidi wa shahidi namba tatu
unaoonyesha mtuhumiwa amekuwa na hatia ya kuua bila kukusudia,”alisema Jaji.
Baada ya kutoa maelezo hayo Jaji Kihwelo, alitoa nafasi kwa Wakili wa wa upande wa Jamhuri, Adolf Maganda, ambaye alidai mtuhumiwa huyo hana rekodi ya makosa ya aina hiyo.
Aliiomba mahakama kutumia kifungu namba 198 cha makosa ya adhabu kilichofanyiwa marekebidho mwaka 2002.
“Mheshimiwa Jaji ninaiomba mahakama yako tukufu impe adhabu mtuhumiwa, ikiwezekana kifungo cha maisha gerezani,” alisema Wakili Maganda.
Baada ya Wakili Maganda kutoa maelezo yake, Jaji Kihwelo alitoa nafasi kwa Wakili wa upande wa utetezi, Rwezaura Kaijage kuzungumza na mteja wake kwa muda mfupi kabla ya kutolewa adhabu.
Wakili Kaijage, alisema kwa kuwa mahakama imeshamtia hatiani mshtakiwa kwa kuona ameua bila kukusudia na kwa kupitia maombi ya mshtakiwa kutaka apunguziwe adhabu.
“Mheshimiwa Jaji, mtuhumiwa ni kijana mdogo mwenye umri wa miaka 27 na bado taifa linamtegemea.
“Katika operesheni iliyofanyika Septemba 2, mwaka 2012 ambako ndipo maafa hayo yalipotokea hakwenda kwa idhini yake bali alikuwa akifanya hivyo kwa kuwa wao hufanya kazi
kwa amri.
“Silaha iliyotumika ilijifyatua kwa bahati mbaya, mtuhumiwa hakuwa na uwezo wa kuizuia kwa kuwa lilikuwa nje ya uwezo wake.
“Mshtakiwa ameshakaa mahabusu kwa miaka minne na katika kipindi hicho amekwishajutia kosa alilolitenda,” alidai Wakili Kaigaje.
Wakili huyo wa utetezi alisema wazazi wote wa mshitakiwa wamekwisha kufariki dunia hivyo ana jukumu la kuwalea wadogo zake watano walioachwa pamoja na mtoto wake mdogo mwenye umri wa miaka mitano.
Baada ya kusikiliza hoja hizo Jaji Kihwelo aliahirisha kesi hiyo hadi kesho kwa ajili ya kutoa adhabu kwa mshtakiwa aliyetiwa hatiani.
0 comments:
Post a Comment