WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema atahamia Dodoma ifikapo Septemba, mwaka
huu kuonyesha kuwa Serikali imedhamiria kutekeleza ahadi ilizotoa kwa
wananchi.
Ametoa kauli hiyo leo asubuhi (Jumatatu, Julai 25,
2016) wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa mkoa wa Dodoma na
kuwashukuru kwa ushiriki wao kwenye maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya
Mashujaa zilizofanyika kwenye uwanja wa Mashujaa, mjini Dodoma.
“Jana
nilimwita Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu na kumwambia akamilishe
matengenezo kwenye nyumba yangu kwa sababu ninataka kuhamia Dodoma
ifikapo Septemba,” amesema na kushangiliwa na mamia ya wakazi wa mji wa
Dodoma waliohudhuria maadhimisho hayo.
Amesema tangu Serikali ya
awamu ya tano iingie madarakani, kazi nyingi zimefanyika na wananchi
wameziona na kwamba sasa hivi kazi iliyobakia ni utekelezaji wa ahadi
alizotoa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John
Magufuli.
“Wananchi kazi mmeziona na sasa tunaenda kwenye
utekelezaji. Ninatoa agizo kuwa mawaziri na manaibu wote wahame mara
moja kutoka Dar es Salaam na kuja Dodoma. Wana ofisi ndogo Dodoma na kwa
kuwa wamekuwa wakiishi wakati wote wa Bunge, wahamie mara moja. Mimi
nahamia Septemba, na utekelezaji wake nitausimamia kwa juhudi zote,”
alisisitiza.
Amewataka wakazi wa Dodoma watumie fursa hiyo kutunza
amani ya nchi na kudumisha umoja uliopo na pia akataka watumie fursa
hiyo kujenga nyumba za kuishi za kutosha, nyumba za kulala wageni na
hoteli za kitalii ili watu watumishi na wageni wanapokuja wasipate taabu
mahali pa kuishi.
Wakati huo huo, mgeni rasmi kwenye maadhimisho
hayo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli katika
muda wa siku tatu amerudia kusisitiza nia ya Serikali kuhamia Dodoma
katika kipindi chake cha uongozi ili kutekeleza ndoto ya hayati Baba wa
Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya kutaka makao makuu ya nchi
yawe Dodoma.
Akizungumza na mamia ya wakazi wa mji wa Dodoma kwenye
uwanja wa mashujaa huku akishangiliwa, Rais Magufuli amesema
atahakikisha Dodoma inakuwa makao makuu ndani ya miaka minne na miezi
minne iliyobakia kwenye awamu ya kwnza ya uongozi wake.
“Kama wabunge
karibu 300 na mawaziri na manaibu wao ambao hawafiki 30 wanakaa hapa
kwa miezi mitatu na maisha yanakwenda, kama makao makuu ya chama
kinachotawala nchi yako hapa sioni sababu ni kwa nini Serikali
ninayoiongoza iendelee kubakia Dar es Salaam,” amesema.
Mara kwanza
kutoa kauli hiyo, ilikuwa ni Jumamosi iliyopita, Julai 23, 2016 wakati
akitoa hotuba yake ya kwanza mara baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti
wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Mkutano Mkuu maalum wa chama hicho.
Rais
Magufuli amesisitiza wananchi na wanasiasa kutunza amani na kudumisha
amani iliyokuwepo nchini. Pia amewataka Watanzania wote kuendelea
kuwaenzi mashujaa walioipigania nchi hii.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment