UKISTAAJABU ya Mussa utayaona ya Firauni. Ndivyo unaweza kusema baada ya Polisi Mkoa wa Morogoro kumtia mbaroni Benjamin Zakaria kwa tuhuma ya kuingia katika hospitali ya mkoa na kujifanya daktari ndani ya wodi ya wagonjwa mahututi.
Akiwa
ndani ya hospitali hiyo, Zakaria anadaiwa alijifanya daktari mgeni na
kuanza kukagua huduma zinazotolewa na hospitali hiyo.
Zakaria ambaye
ni mkazi wa Tungi mjini hapa, aliingia katika hospitali hiyo na kuvaa
vazi la kidaktari, kisha kutembelea wodi mbalimbali akiwahoji wagonjwa
waliokuwa wamelazwa hospitalini hapo.
Akizungumza na waandishi wa
habari kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich
Matei, alisema kuwa daktari huyo feki alitiwa mbaroni baada kutiliwa
shaka na muuguzi wa zamu katika hospitali hiyo, ambaye alitoa taarifa
polisi.
“Alifika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro na
kujifanya kama madaktari wengine waliokuwa wakiendelea kutoa huduma kwa
wagonjwa. Alipofika wodi ya wagonjwa mahututi, alikutana na muuguzi wa
zamu na kudai yeye ni daktari mgeni.
“Hata hivyo, muuguzi huyo alimtilia shaka na aliufahamisha uongozi wa hospitali juu ya uwepo wa daktari huyo feki, na kisha tukafahamishwa polisi na kufanikiwa kumkamata,” alisema Kamanda Matei.
Mmoja
wa wauguzi katika wodi ya wagonjwa mahututi, Expiransa Mtama, alisema
kuwa alibaini daktari huyo feki hana sifa za kitabibu baada ya kumuhoji
maswali ya kina ya kitaalamu ambayo alishindwa kuyajibu.
Tukio hilo
ni la pili kutokea hospitalini hapo baada ya Julai 12, 2014, kijana
mwingine mkazi wa Liti, Manispaa ya Morogoro, Karume Kauzu, kukamatwa
kwa tuhuma za kujifanya daktari.
Kijana huyo ambaye ni mwenyeji wa Mkoa wa Kigoma, alikamatwa na uongozi wa hospitali hiyo baada ya muuguzi mmoja aliyekuwa zamu, kumuhisi hakuwa daktari wa kweli, na kuamua kutoa taarifa kwa uongozi.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment