JESHI
la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limemkamata Askofu wa Kanisa
la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere (JNIA), baada ya kushuka katika ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (Kenya Airways) akitokea nchini Kenya.
Askofu
Gwajima, alikamatwa jana asubuhi na makachero wa Jeshi la Polisi
waliokuwa wamepiga kambi eneo hilo, baada ya kupata taarifa za kuwasili
kwake.
Vyanzo vya habari kutoka kwa watu wa karibu na Askofu Gwajima,
viliiambia MTANZANIA kuwa baada ya kiongozi huyo wa kiroho kushuka
katika ndege, alitakiwa kupanda helikopta yake ili aelekee Hoteli ya Sea
Cliff iliyopo Masaki, Dar es Salaam kwa ajili ya mapumziko.
Kabla ya kuanza safari ya kuelekea
Sea Cliff, Askofu Gwajima, alijikuta akiishia mikononi mwa polisi na
kupelekwa moja kwa moja Kituo Kikuu cha Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam kwa ajili ya kuhojiwa.
Vyanzo hivyo vilidai kuwa baada ya
kufikishwa kituoni, alipelekwa kwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya
Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro na baadaye ofisi ya Mkuu wa
Upelelezi wa kanda hiyo, Camillus Wambura.
“Askofu Gwajima alikamatwa
uwanja wa ndege na polisi akitokea nje ya nchi na kufikishwa Kituo
Kikuu cha Polisi cha Kanda Maalumu na kuhojiwa, lakini ameachiwa kwa
dhamana na simu zake za kiganjani zinashikiliwa kwa ajili ya
uchunguzi,” kilisema chanzo hicho.
MTANZANIA ilipomtafuta msemaji wa kiongozi huyo wa kiroho, Yekonia Behagaze, ili kuzungumzia suala hilo, alikiri kiongozi wao kukamatwa.
“Ni kweli Askofu Gwajima amekamatwa na polisi leo (jana) asubuhi akitokea nje ya nchi, alihojiwa kwa saa nne,” alisema.
Alisema baada ya kumaliza mahojiano hayo, aliachiwa kwa dhamana ili aendelee na majukumu yake.
Kamanda
wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Sirro, alipoulizwa
na MTANZANIA, alithibitisha kukamatwa kwa Askofu Gwajima.
“Ameletwa, amehojiwa, amepewa dhamana na uchunguzi unaendelea,” alisema.
Jeshi
la Polisi lilianza kumtafuta Askofu Gwajima tangu Juni 16, mwaka huu,
baada ya askari kuzingira nyumba yake iliyopo eneo la Salasala.
Sababu kubwa ya kutafutwa Askofu Gwajima ni kwa ajili ya kuhojiwa juu ya mahubiri yake aliyoyatoa kanisani kwake Ubungo Maji, Juni 11, mwaka huu.
Katika mahubiri hayo
ambayo yalisambazwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, Askofu
Gwajima alisikika akikosoa utendaji kazi wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Pia
alisikika akimshauri Rais Dk. John Magufuli, kuhama Chama Cha Mapinduzi
(CCM) iwapo watakataa kumkabidhi uenyekiti wa chama hicho.
Alidai
kama ikishindikana, basi Magufuli apeleke muswada bungeni kuondoa kinga
ya rais ili Kikwete ashtakiwe kwa makosa aliyoyafanya akiwa madarakani.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment