WAKAZI
wa Dodoma jana asubuhi waliingiwa na taharuki baada ya mji huo kukumbwa
na tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa kipimo cha Richter 5.1.
Akizungumza
jana ofisini kwake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Jiolojia Tanzania,
Profesa Abdulkarim Mruma alisema tetemeko hilo lililotokea saa 12.01:15
asubuhi wakati wananchi wengi wakiwa wamelala na ni kubwa ukilinganisha
na matetemeko ambayo yamezoeleka kutokea yenye ukubwa wa Richter 3.
Profesa Mruma alisema kitovu cha tetemeko hilo kilikuwa katika Bonde la Haneti - Itiso wilayani Chemba mkoani Dodoma.
Pia
alisema kutokana na ukubwa wa tetemeko hilo, mikoa mingine ambayo ipo
karibu na eneo la chanzo cha tetemeko nayo imeathirika na kuitaja mikoa
hiyo iliyoathirika kuwa ni pamoja na Tanga, Dodoma, Singida upande wa
mashariki na Manyara.
Alisema tetemeko hutokea katika miamba migumu
yenye madini ya dhahabu. Akielezea chanzo cha tetemeko, Profesa Mruma
alisema limesababishwa na kupasuka kwa matabaka ya ardhi, na hutokea
kutokana na kuteleza kwa mapande hayo ambapo husababisha mtikisiko.
Alisema
mapande ya ardhi ya Itiso ambayo yapo katika mtawanyiko wa Bonde la Ufa
la Arusha yanaendeleza kuteleza na kwamba tetemeko hilo ni endelevu
kwani bonde hilo la Itiso linazidi kusogea.
Alishauri watu wanaojenga
maghorofa katika mkoa wa Dodoma kuzingatia ushauri wa Wakala wa
Jiolojia, kwani athari za kujenga majengo marefu kwa mkoa huo bado zipo
pale pale.
Aliwataka wanaojenga ghorofa waombe ushauri kwao kwani ukitaka kujenga ghorofa zaidi ya mbili ni lazima jengo liwe pana.
Kwa
upande wa Mjiolojia Mwandamizi kutoka Wakala wa Jiolojia Tanzania
ambaye pia ni mtaalamu wa matetemeko, Gabriel Mbogoni alisema tetemeko
hilo limetokea maeneo ya Haneti kilometa 11 mashariki mwa mji wa Haneti
Wilaya ya Chemba ambao upo kilometa 79 kutoka kaskazini mashariki mwa
mji wa Dodoma.
“Hatujapata taarifa zozote za madhara labda kwa sababu bado ni mapema,” alisema Mbogoni.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment