Image
Image

Kongole TFF kumaliza mvutano Stand United

SIKU zote migogoro ni moja ya vyanzo vinavyorudisha nyuma maendeleo ya soka katika ngazi ya klabu au nchi hasa ukanda huu wa Afrika Mashariki.
Kunapokuwa na mgogoro suala la maendeleo linakuwa gumu kuzungumzika katika sehemu yoyote hata kwenye ngazi ya familia.
Hivi karibuni klabu ya Stand United ya mkoani Shinyanga ilifanya uchaguzi kwa lengo la kuwapata viongozi wake watakaoiongoza timu hiyo iliyopanda daraja msimu wa 2014/2015 na kucheza ligi kuu msimu uliopita.
Uchaguzi huo uliibua mgogoro ndani ya klabu hiyo kutokana na mgawanyiko uliotokea huku upande mmoja ukidai timu hiyo ni kampuni na iendeshwe kwa mfumo wa kampuni na kundi lingine likipinga jambo hilo hali iliyopelekea uchaguzi huo kugubikwa na ‘sintofahamu’.
Mvutano wa pande hizo ulipekekea Shirikisho la soka nchini kutangaza kutotambua uhalali wa uchaguzi huo na kuzidi kukoleza fukuto la mgogolo ndani ya klabu hiyo.
Nipashe tunaipongeza TFF kwa busara walizotumia mpaka kufikia muafaka wa jambo hilo nyeti.
Kitendo cha TFF kukiri kuhusika na mgogolo huo ambao umedumu ndani ya klabu hiyo kwa kipindi cha miaka miwili hakika ndio kulitoa mwanga wa kutafuta muafaka na kulimaza jambo hilo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Revocatus Kuuli alikili jambo hilo na kuahidi kulitafutia ufumbuzi jambo ambalo amelifanikisha.
TFF wiki iliyopita ilitangaza kuutambua uchaguzi wa klabu hiyo na kuwapa baraka zote viongozi waliochaguliwa na hiyo ilitokana na Mwenyekiti huyo kulifuatilia jambo hilo kwa kina.
Kuuli amefanya jambo jema kwa kukutana na pande zote na baadae kurejesha ripoti TFF na kufanyia kazi mapungufu aliyoyaona kwenye mchakato mzima wa uchaguzi.
Hata mashabiki wa klabu hiyo wamenukuliwa kuipongeza TFF kwa kumaliza sakata hilo ambalo linaonekana lilikuwa kikwazo kwa klabu hiyo kupiga hatua katika maendeleo yake.
Mgogolo huo wa viongozi ulihakisi mpaka kwenye timu kwa maana ya wachezaji na mwalimu ambapo mara kwa mara tulisika mvutano wa baadhi ya wachezaji na kocha wao ambao ulichangia timu kutofanya vizuri.
Baada ya mambo hayo kumalizika, tunaamini sasa mpira utachezwa huku pande zote zilizokuwa na mvutano zikishirikiana kuifanya Stand United kuwa timu hatari na yenye mafanikio kwenye ligi kuanzia msimu ujao.
Lazima pande hizo zifahamu kuwa wote wanajenga nyumba moja hivyo hakuna haja ya kugombania fito, sasa ni wakati wa kukaa pamoja na kusuka mikakati ya kuifanya Stand kuwa moja ya timu bora msimu ujao.
Mshikamano kati ya wanachama, viongozi na wachezaji vinasaidia kuifanya timu kupata mafanikio na mifano hiyo ipo wazi.
Mfano wa karibu zaidi, kwa sasa Yanga ni timu inayofanya vizuri zaidi nchini, imefanikiwa kutwaa tuzo zote msimu huu kuanzia ngao ya Hisani, Kombe la Shirikisho (FA) na ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara huku pia ikifanikiwa kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, mafanikio haya yote yamechagizwa na utulivu ndani ya klabu hiyo kuanzia wanachama, viongozi mpaka benchi la ufundi.
Kuna haja ya klabu nyingine nchini zijifunze hapo hasa suala la umoja na mshikamano kwa sababu ndio sababu ya msingi Yanga kufanya vizuri.
Na kwa TFF isiishie kwa Stand United peke yake, tayari kwa sasa kuna mvutano ndani ya Chama cha soka Manispaa ya Kinondoni unaotakana na matokeo ya Uchaguzi wao uliofanyika Juni 12 mwaka huu.
TFF imetangaza kutowatambua viongozi waliopo madarakani na hiyo ni baada ya mmoja wa wagombea aliyeshindwa kwenye nafasi ya Mwenyekiti wa Chama hicho kuamua kwenda kushataki ndani ya Shirikisho hilo.
Nipashe tunaishauri TFF kutumia njia waliyoitumia kumaliza mgogoro wa Stand United pia kumaliza suala hili la Chama cha Soka Wilaya ya Kinondoni ( KIFA) kilichoko jijini Dar es Salaam.
Mpira unahitaji mipango ya muda mrefu hivyo kuwa na mvutano ndani ya timu au chama cha soka ni wazi hakutakuwa na mipango yoyote ya kukuza na kuendeleza mpira nchini.
Kwa mara nyingine, tunaipongeza TFF na Kamati yake ya Uchaguzi kumaliza suala la Stand United, lakini sasa waligeukie suala la uongozi ndani ya KIFA ili kuondoa msuguano wowote na kuacha soka lichezwe.
KIFA ikitulia, tutashuhudia mashindano mbalimbali yakifanyika kwenye wilaya hiyo
ambayo ilikuwa kinara kuzalisha wachezaji wa Timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) kutokana na ligi waliyokuwa wanaiendesha.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment