KIKOSI
cha Usalama Barabarani kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa
Usafiri Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) zimezifungia kutoa huduma kampuni
tatu za mabasi yaendayo mikoani, ikiwemo ya City Boy.
Kampuni nyingine zilizokumbwa
na hatua hiyo ya kulinda mali na usalama wa raia ni pamoja na Super
Sami na Otta High Class. Wakati mabasi ya City Boy yakifungiwa kutokana
na ajali ya mabasi yake mawili kugongana yakiwa safarini kwa uzembe wa
madareva Jumanne wiki hii na kupoteza maisha ya abiria wapatao 30 na
kujeruhi watu wapatao 48, mabasi ya Super Sami na Otta nayo katika
kipindi cha wiki moja zilihusika katika ajali tatu ambazo pia zilipoteza
maisha ya watu 46 na majeruhi 73.
Inasikitisha kuona mwenendo huu
ukizidi kuota mizizi na kuwafanya Watanzania kuanza kuzoea kusikia juu
ya mabasi yetu ya abiria yakisababisha ajali na kupoteza maisha ya watu
na majeruhi karibu kila kukicha.
Sisi tunapenda kutoa pongezi kwa
wenzetu wa Usalama Barabarani na SUMATRA kwa kuchukua hatua za
kuzifungia kampuni hizo na wahusika, kwa maana ya madereva, ili nao wafikishwe kwenye vyombo vya sheria waweze kupata wanachostahili kutokana na uzembe wa kuchezea maisha ya abiria.
Tungependa
kuvikumbusha pia vyombo vya dola kufikiria upya juu ya suala zima la
utoaji leseni kwa madereva wa mabasi ya abiria na hata namna ya
upatikanaji wa madereva husika ili kujiridhisha na ubora wa kazi zao,
umri wa kuwajibika ipasavyo wawapo safarini badala la kujitwika viroba
na pombe nyingine wakiwa kazini lakini pia kuwepo na madereva wa
kupokezana kwa wale wanaosafiri umbali mrefu.
Tunapenda kusisitiza
kwamba, kwa jambo hili hakuna njia ya mkato lazima wadau katika sekta
hiyo ya usafiri wakiwemo wamiliki mabasi, Usalama Barabarani, SUMATRA na
hata wananchi wa kawaida kwa maana ya abiria, nao washirikishwe katika
kutafuta njia bora ya kupata suluhu ya ajali za barabarani.
Hakuna
ubishi kwamba, hivi sasa tunatengeneza yatima, wajane, wagani na vilema
wengi ambao kwa kila hali, jamii nzima inatugusa kutokana na ukweli
kwamba waliokuwa na baba, mama na jamaa zao sasa wako katika shida
kubwa, kisa ni uzembe wa madereva wasiotaka kusikia ya wataalamu wa sheria na taratibu ambazo wanazihamu fika.
Ni
kweli kwamba ajali haina kinga, lakini ni ukweli pia kwamba mabasi
yanayokwenda zaidi ya kasi ya mwendo wa kilometa 80 kwa saa yapo katika
hatari kubwa zaidi ya kupata ajali kuliko ambayo madereva wake
wanazingatia mwendo huo pamoja na alama za barabara.
Udhibiti wa uhai
wetu tukiwa barabarani uko katika mikono ya madereva wetu na abiria
wenyewe. Upo uwezekano wa kusafiri na kuwa salama kama kila mmoja wetu
atachukua hatua pale panapohitajika kumripoti dereva anayeendesha kwa
mwendo wa kifo kwa kupiga simu polisi ili hatua zichukuliwe dhidi ya
dereva husika. Hivi tutaendelea kulia hadi lini? Haitusaidii ni lazima
tuchukue hatua dhidi ya kadhia hii ya ajali.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment