WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema uamuzi wa Serikali kuhamia siyo siasa kama
watu wanavyodhani bali ni utekelezaji wa maamuzi kamili na kwamba
Serikali inakamilisha eneo la kisheria juu ya uamuzi huo.
“Hapa
tulipofika ni hatua ya utekelezaji wa pamoja na hakuna namna nyingine
kwa sababu uamuzi umeshatolewa. Nataka niwahakikishie kwamba hii siyo
siasa, tunachokamilisha ni eneo dogo tu la kisheria juu ya uhamishaji wa
makao makuu kuja Dodoma na katika Bunge la Septemba sheria hii
itapitishwa,” amesema.
Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumanne, Julai
26, 2016) wakati akizungumza na viongozi wa mkoa, Serikali za mitaa,
viongozi wa dini, wajasiriamali, wazee wa mji huo, wasafirishaji,
wafanyabiashara, wakuu wa taasisi za elimu, za kifedha na watoa huduma
mbalimbali katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Hazina ndogo
mjini Dodoma.
Waziri mkuu ambaye aliitisha kikao cha kazi na wadau
hao mjini Dodoma, ameutaka uongozi wa mkoa huo pamoja na wadau wake
wakae na kuandaa mpango kazi wa jinsi ya kupokea na kutekeleza uamuzi wa
Serikali kuhamia Dodoma.
Pia ametoa siku 14 kwa uongozi wa mkoa wa
Dodoma kukamilisha mpango kazi wao na kumkabidhi mapendekezo yao ili
yaweze kuingizwa kwenye mpango mkubwa wa Serikali kuu.
“Uongozi wa
Mkoa, ukishirikiana na Ofisi yangu kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu na Ofisi ya Rais TAMISEMI usimamie na kuyaratibu majukumu
haya. Ndani ya siku 14 nipate proposal ya kwanza namna
mtakavyoyatekeleza. Naagiza kiundwe kikosi kazi chini yenu
kitakachowajumuisha makundi yote niliyoyataja,” amesema Waziri Mkuu.
Waziri
Mkuu amesema chimbuko la uamuzi wa kuhamia Dodoma kuifanya makao makuu
ya Serikali lilikuwa ni ndoto ya Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage
Nyerere ambayo imeendelea kudumu katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha
Mapinduzi ikiwemo Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015 chini ya Ibara ya 151.
“Napenda
kumshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan,
na viongozi wengine wote wa Chama kwa kusimamia ndoto ya Baba wa Taifa
ya kuhamishia Makao Makuu hapa Dodoma. Ni imani yangu kuwa wananchi
wote mtaunga mkono uamuzi huu muhimu kwa Serikali yetu na wananchi kwa
ujumla, amesema.
Akiweka msisitizo juu ya kazi kubwa inayowakabili
viongozi hao, Waziri Mkuu amesema masuala yanayotakiwa kufanyika kuanzia
sasa ni pamoja na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kuhakikisha
eneo la makazi ya Serikali Kuu litakalotumika kwa ofisi za wizara na
taasisi zake, makazi ya watumishi na huduma za biashara elimu na
taratibu zote za kisheria za kulitwaa zinakamilika kwa haraka na
linakuwa tayari kwa matumizi.
“Natambua kazi iliyopo mbele yetu ni
kubwa na inahitaji jitihada za pamoja. Hivyo kila taasisi na mtu mmoja
mmoja ana jukumu la kuhakikisha kuwa tunajipanga vizuri na kuweka
mazingira ya ujio wa Serikali katika maeneo yote muhimu,” amesema.
Amezitaka
Mamlaka za Mipango Miji na hasa CDA wahakikishe wanaweka mfumo mmoja wa
upatikanaji wa viwanja ambao utajulikana na kila mmoja, utakuwa wazi
usio na urasimu. “Mfumo huu wa viwanja uwekwe kwenye mfumo wa kompyuta
na uuzaji wa viwanja hivyo uwe wa kieletroniki kuepusha udanganyifu
kutoka kwa madalali,” amesisitiza.
Waziri Mkuu ameonya CDA na
Manispaa zisibadili ramani ya mipango miji iliyokwishawekwa awali kama
vile maeneo ya wazi kutumika tofauti na makusudio yaliyokusudiwa na
akaagiza maeneo hayo yote yarejeshwe na kufufuliwa.
“Natambua katika
makazi hapa Dodoma kulitengwa maeneo ya vituo maalum vijulikanavyo kama D
Centers kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali. Cha ajabu sasa kuna
magenge, groceries na sasa naagiza kwa hadhi ya Makao Makuu haya maeneo
sasa yatumike kuwekeza maduka makubwa (shopping malls) ambamo huduma
zote mbalimbali hupatikana,” amesema.
Ameitaka Manispaa iboresha
usafi wa mazingira na bustani zake kwa kushirikiana na taasisi
mbalimbali kuzitunza. Pia ameitaka manispaa ya mji huo ishirikiane na
TANROADS kuboresha barabara zote za mitaa na taa za barabarani mji ukae
kisasa, na usalama uwe bora zaidi.
“Eneo jingine muhimu ni Manispaa
na CDA kuhamisha makundi mbalimbali ya wafanyabiasahra na huduma za
masoko yasiyo rasmi na kuyapa maeneo yaliyo rasmi na bora zaidi. Hii ni
pamoja na maeneo ya maegesho ya bajaji, bodaboda, taxi na daladala. Pia
mazingira ya Stendi Kuu yaboreshwe, vyoo vya kulipia pia vijengwe
katikati ya mji,” amesisitiza.
Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa
Wakala wa majengo (TBA) waorodheshe majengo yote ya Serikali na taasisi
zake yanayotumika kwa sasa na yasiyotumika, “Nataka muyawekee utaratibu
maalum wa matumizi yake ili tupate kujua yanayoweza kutumika kwa muda
kwa baadhi ya wizara na taasisi zake. Hii ni pamoja na jengo jipya la
Mkuu wa Mkoa, linaloendelea kujengwa.”
Amewataka wakazi wa Dodoma
watumie fursa hiyo kujenga nyumba za kuishi za kutosha, nyumba za kulala
wageni na mahoteli ili watu watumishi na wageni wanapokuja wasipate
taabu mahali pa kuishi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment