JESHI
la Polisi mkoani Arusha linatarajia kuwahoji wabunge wawili, Mwenyekiti
wa Halmashauri na makamu wake wote kutoka Chadema, baada ya kufanya
mikutano ya hadhara 14.
Viongozi hao wametakiwa kufika ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha (RCO) kwa ajili ya kuhojiwa.
Wabunge
walioandikiwa barua na kutakiwa kufika ofisini kwa RCO jana ni Mbunge
wa Karatu, Wilbroad Qambalo, Mbunge wa Viti Maalumu, Cecilia Pareso,
Mwenyekiti wa Halmashauri, Jublet Munyenye na makamu wake, Lazaro
Bajuta.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Pareso alikiri kupokea barua
yenye kumbukumbu namba KRT/CID/B1/7H/VOL.VIII/344 kutoka ofisi ya Mkuu
wa Upelelezi Wilaya ya Karatu ya Julai 25, mwaka huu.
Alisema barua
hiyo inamtaka yeye na viongozi wenzake waliokuwa kwenye mkutano wa
hadhara Julai 23, mwaka huu katika Kitongoji cha Ganako Kijiji cha Tloma
Kata ya Ganako, wafike ofisini kwa RCO Julai 25, mwaka huu saa 8.00
mchana kwa ajili ya mahojiano.
“Nimepokea barua mchana huu Saa 6:30
(jana) nikiwa hapa Karatu, sasa siwezi kukurupuka kuanza safari ya
kwenda Arusha, nina ratiba zangu.
“Karatu mpaka Arusha mjini kuna
mwendo mrefu, kama wao wameniletea barua saa 6:30 mchana nawezaje kufika
Arusha mjini saa 8.00 mchana. Nitakwenda ofisini kwa RCO Jumatano saa
4.00 asubuhi,” alisema.
Alisema analishangaa jeshi hilo kwa sababu mbunge ana mamlaka ya kuzungumza na wananchi wake kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Alisema mkutano huo ulioitishwa na Qambalo ulilenga kusikiliza kero za wananchi na kuhimiza shughuli za maendeleo.
Munyenye
alipoulizwa kuhusu taarifa hiyo, alikiri kuipokea huku akilishangaa
jeshi la polisi wilayani humo kufanya kazi bila weledi.
“Huu ni
usumbufu usio kuwa na msingi, jeshi la polisi limeacha kufanya kazi kwa
maadili yake badala yake sasa wanataka kujipendekeza kwa viongozi kuwa
wapo makini,” alisema.
Kutokana na kadhia hiyo, walimpigia Waziri wa
Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba na kumtaka awape ufafanuzi wa mbunge wa
jimbo kufanya mikutano ya hadhara.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Yusuf Ilembo, alithibitisha viongozi hao kutumiwa barua ya wito.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment