SERIKALI
ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais, John Magufuli imeweka bayana
kwamba itahamia Makao Makuu ya nchi, mjini Dodoma ndani ya miaka minne
iliyobaki.
Rais Magufuli ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya
Ulinzi na Usalama, alitoa msisitizo huo jana kwenye viwanja vya
Mashujaa mjini Dodoma alipokuwa anawasalimia wakazi wa mji huo na
Watanzania kwa ujumla wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mashujaa.
Tunapenda
kumpongeza Rais katika salamu zake kwa kutoa angalizo kwamba
atahakikisha serikali yote inahamia Dodoma bila kukosa na kuwataka
viongozi wengine kuacha kutoa visingizio.
Pongezi hizo tunapenda pia
zimwendee Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye alipopewa nafasi ya
kuzungumza katika tukio hilo naye kwa upande wake alitangaza kuwa
atahamishia ofisi yake mjini Dodoma mwezi Septemba, mwaka huu.
Waziri Mkuu hakuishia hapo pia aliweka bayana kuwa akishatangulia kwenda Dodoma, mawaziri wote na manaibu wao, nao watamfuata.
Ama
kweli Hapa kazi Tu! Hakuna ubishi kwamba awamu zote zilizotangulia
zilikuwa na mikakati mbalimbali ya kutaka kuhamia makao makuu ya nchi
mjini Dodoma lakini sote ni mashuhuda kwamba azma hiyo haikutimizwa
kutokana na sababu mbalimbali.
Sisi tunapenda kurudia pongezi zetu
kwa Rais wa Awamu ya Tano na Serikali yake, kwa kulivalia njuga jambo
hilo na kusisitiza kuwa lazima kuhamishia mawazo hayo katika vitendo.
Hapa tunapenda kutoa mwito kwa wananchi,viongozi wa siasa na serikali
kila mmoja kwa nafasi yake kutoa kila aina ya ushirikiano na mshikamano
ili sote kwa pamoja kuhakikisha kwamba azma hii inatekelezwa bila
kufanya ajizi.
Harakati zozote za kudhoofisha mkakati huo muhimu kwa
Taifa letu zisipewa nafasi wala kusiwepo na kisingizio chochote kile
kama Rais mwenyewe alivyofafanua katika salamu zake. Jambo moja la
muhimu hapa ni kwamba atakayejaribu kwa namna yoyote ile kudhoofisha
juhudi hizo afichuliwe kwenye vyombo husika ili adhibitiwe kwa mujibu wa
sheria na taratibu.
Kwa wakazi wa Dodoma, huo sasa ni wakati wa
kujiandaa kwa maana ya kuwa tayari kwa kuzipokea kwa mikono miwili fursa
zinazokuja mbele yao kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kisiasa. Wakazi
wa Dodoma wasiwe watazamaji bali wawe washiriki kikamilifu katika ujenzi
wa miradi mikubwa ya hoteli za kisasa, nyumba za kupangisha na kufikia
wageni, utalii, migahawa na maeneo ya burudani.
Hakuna ubishi kwamba
Dodoma ya miaka minne ijayo itakuwa na utofauti wa aina yake katika
nyanja zote za kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. Masuala ya kuboresha
miundombinu ili iendane na mahitaji ya idadi ya watu na ofisi za
serikali na watumishi wake nayo yana umuhimu wa pekee.
Barabara
ziboreshwe kwa viwango vya lami, usambazaji wa umeme, maji na masoko
navyo vipewe kipaumbele kinachostahiki ili kutekeleza kwa ufanisi zoezi
zima la serikali nzima kuhamia Dodoma. Hayo yote yanawezekana tujipange
kuyatimiza.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment