Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia
salamu za rambirambi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Job Ndugai kufuatia kifo cha Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Kilindi
Mkoani Tanga Mhe. Beatrice Shelukindo kilichotokea jana tarehe 02 Julai,
2016.
Mhe. Beatrice Shelukindo ambaye amewahi kuwa Mbunge Bunge la
Afrika Mashariki na baadaye kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kwa vipindi viwili mfurulizo hadi alipostaafu mwaka jana
2015, amefariki dunia akiwa nyumbani kwao Njiro Mkoani Arusha.
Katika
salamu zake Rais Magufuli amesema taifa limempoteza mtu aliyetoa
mchango mkubwa katika maendeleo hususani alipokuwa Mbunge wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwawakilisha wananchi wa Jimbo la
Kilindi na Mkoa wa Tanga.
“Mhe. Beatrice Shelukindo alikuwa kiongozi
shupavu, ambaye siku zote alisimama kidete kupigania maendeleo ya
wananchi na kutetea rasimali za taifa.
“Kupitia kwako Mhe. Spika Job
Ndugai naomba unifikishie salamu zangu za pole kwa familia, ndugu, jamaa
na marafiki wote wa marehemu na pia kwa wabunge wote wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania” Amesema Rais Magufuli.
Dkt. John Pombe Magufuli
pia amewaombea wote walioguswa na kifo cha Mhe. Beatrice Shelukindo
kuwa na moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hiki cha kuondokewa
na mpendwa wao na amemuombea marehemu apumzishwe mahali pema peponi,
amina.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment