KATIKA
kutekeleza agizo la Rais John Magufuli la kutaka serikali kuhamia
Dodoma, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba amesema
watendaji wa wizara hiyo wataanza kuhamia Dodoma kuanzia wiki ijayo.
Katika
hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa
Justin Ntalikwa amewataka wakuu wa idara na vitengo wote wa wizara hiyo
kuanza maandalizi ya kuhamia Dodoma na kuwa wametekeleza agizo hilo
ifikapo mwezi Septemba, mwaka huu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam
jana, Dk Tizeba alisema tayari watendaji wa wizara hiyo wanaotakiwa
kuhamia Dodoma wameanza kufanya maandalizi ya safari.
Alitoa dokezo
hilo mara baada ya kutoa taarifa kuhusu Mkutano wa Ushirikishwaji wa
Wadau kwenye Sekta ya Uvuvi, unaoishirikisha pia Wizara ya Kilimo,
Maliasili, Mifugo na Uvuvi ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wadau
mbalimbali.
“Ni kweli hata sisi Wizara tuko kwenye maandalizi wiki
hii, kwa sababu wiki ijayo tutahamia Dodoma, tunatekeleza agizo la
Rais,” alisema Waziri Tizeba.
Kauli ya Waziri Tizeba imekuja siku
moja baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutangaza kuhamia Dodoma
ifikapo Septemba mwaka huu, huku akiwataka Mawaziri na Naibu Mawaziri
kumfuata.
Waziri Mkuu alisema ameshaagiza ukarabati kwenye nyumba
yake ukamilishwe ili ifikapo Septemba aweze kuhamia na kuwataka mawaziri
kufanya hivyo kwa sababu kila Waziri ana nyumba na ofisi ndogo mjini
Dodoma.
Nayo Wizara ya Nishati na Madini imetoa waraka ikiwataka
wakuu wa idara na vitengo wote wa wizara hiyo kuanza maandalizi ya
kuhamia Dodoma ifikapo mwezi Septemba mwaka huu.
Agizo hilo lipo
katika waraka uliotolewa na Kabibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini,
Profesa Justin Ntalikwa jana na nakala yake kutumwa pia kwa Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Katibu Mkuu huyo alisema
agizo hilo linatokana na kauli iliyotolewa na Rais Magufuli katika
Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika mjini
Dodoma hivi karibuni, ambapo alisisitiza azma ya serikali yake kuhamia
Dodoma.
Alisema pamoja na kauli ya Rais, watendaji hao wanatakiwa
kuanza maandalizi ya kuhamia Dodoma ifikapo Septemba kutokana na Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa kuahidi kuhamia Dodoma mwezi huo na kuwataka
Mawaziri na Naibu Mawaziri nao kumfuata.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment