WAFANYABIASHARA
wawili, akiwemo Mohamed Yusufali “Choma”, wamepandishwa kizimbani
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka 222 ya
kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 14.
Mbali na
Yusufali aliyewahi kutajwa kuwa anajipatia Sh milioni saba kwa dakika
moja kwa njia ya udanganyifu katika mapato ya serikali, mshitakiwa
mwingine ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Northern Engineering Works Limited,
Samwel Lema, ambao wanadaiwa kusababisha hasara kwa kughushi na kukwepa
kulipa kodi.
Washitakiwa walifikishwa mahakamani hapo jana na
kusomewa mashitaka kwa zaidi ya saa tatu na Wakili Mwandamizi wa
Serikali, Mutalemwa Kishenyi, akisaidiwa na Jackline Nyantori, Diana
Lukondo na Wakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru), Leonard Swai.
Mbele ya Hakimu Mkazi Wilbard Mashauri,
ilidaiwa, katika tarehe tofauti kati ya Januari Mosi 2012 na Desemba 31,
2014, washitakiwa hao na wengine ambao hawajafikishwa mahakamani
walipanga njama za kuidanganya Mamlaka ya Mapato (TRA) na kujipatia Sh
14,052,011,435.
Wakili Kishenyi akisaidiwa na Nyantori walidai,
katika shitaka la tano hadi 103 kuwa, kati ya mwaka 2011 na 2013, jijini
Dar es Salaam na Arusha, washitakiwa hao walighushi stakabadhi za
malipo kuonesha Kampuni ya Northern Engineering Works Ltd imenunua
bidhaa mbalimbali.
Ilidaiwa kuwa stakabadhi hizo zilionesha kuwa
kampuni hiyo imenunua bidhaa mbalimbali kutoka kwenye kampuni tofauti
tofauti ikiwemo ya Festive General Business Ltd, Ever Global General
Trading na Jambo Product Ltd, jambo ambalo si kweli.
Wakili Diana na
Swai waliendelea kudai, katika shitaka la 104 hadi 141, kuwa kati ya
mwaka 2011 na 2015, Lema alighushi hati ya Kodi ya Ongezeko la Thamani
(VAT) kuonesha kuwa kampuni yake imenunua bidhaa mbalimbali kutoka
kampuni tofauti tofauti ikiwemo ununuzi wa vifaa vya Sh bilioni 1.7.
Wakili
Swai alidai katika shitaka la 142 hadi 219 kuwa, kwa lengo la kufanya
udanganyifu washitakiwa hao walighushi stakabadhi za malipo kuonesha
Kampuni ya Elerai Constructions Ltd, imenunua vifaa mbalimbali kutoka
katika kampuni tofauti tofauti ikiwemo Kampuni ya Blue Arrow Tanzania
Ltd.
Aliendelea kudai shitaka la 220, linamkabili Lema ambaye
anadaiwa kati ya Januari Mosi, 2012 na Desemba 31, 2015, Dar es Salaam,
akiwa Mkurugenzi anayehusika kushughulikia Kampuni yake ya Northern
Engineering Works Ltd na Elerai Constructions Ltd zilizosajiliwa kama
walipa kodi, aliwasilisha nyaraka za uongo.
Inadaiwa aliwasilisha
nyaraka ambazo ni marejesho ya uongo ya Kodi ya VAT kwa Kamishna Mkuu wa
TRA jambo lililosababisha akwepe kulipa kodi ya Sh bilioni
14,052,011,435.
Katika mashitaka ya utakatishaji wa fedha, ilidaiwa
kati ya Februari Mosi, 2012 na Februari 25, 2013 jijini Dar es Salaam na
Arusha, washitakiwa hao walijihusisha na kuhamisha Sh milioni 420
zilizotokana na vitendo vya uhalifu.
Inadaiwa waliziingiza fedha hizo
kwenye akaunti namba 1010000541 inayomilikiwa na Iqbal Jaferali
Jafferjee iliyopo katika Benki ya I&M tawi la Kariakoo, na kuzitoa
huku wakijua zimepatikana kwa njia za uhalifu ambazo ni kughushi na
kukwepa kulipa kodi.
Iliendelea kudaiwa katika shitaka la 222 kuwa,
kati ya Januari Mosi, 2012 na Desemba 31, 2015, Dar es salaam, kutokana
na vitendo vyao vya kuwasilisha marejesho ya VAT ya uongo kwa Kamishna
Mkuu wa TRA waliisababishia mamlaka hiyo hasara ya zaidi ya Sh bilioni
14.
Hakimu Mashauri aliwaeleza washitakiwa hao kuwa, hawaruhusiwi
kujibu mashitaka yao kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza
kesi za uhujumu uchumi isipokuwa Mahakama Kuu.
Baada ya kusomewa
mashitaka, upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo bado
unaendelea na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa, hata hivyo Wakili Alex
Mgongolwa anayeongoza jopo la Mawakili wa Utetezi aliomba kuwasilisha
ombi.
Aliiomba Mahakama ifute shitaka la utakatishaji wa fedha kwa
kuwa lina mapungufu makubwa ya kisheria ambayo hayawezi kurekebishwa
wala kufumbiwa macho isipokuwa kufutwa.
Alidai ili shitaka liwe la
utakatishaji wa fedha lazima kuwa na dhamira ya kuficha chanzo cha fedha
au lengo la washitakiwa kukwepa adhabu lakini kama hakuna mambo hayo
sheria inatoa mamlaka kwa Mahakama kuyafuta mashitaka hayo.
Upande wa
Jamhuri uliiomba Mahakama iahirishe kesi hiyo ili wajiandae kujibu hoja
za upande wa utetezi. Hakimu Mashauri alikubali ombi hilo na kuahirisha
kesi hiyo hadi kesho kwa ajili ya kusikiliza majibu ya Jamhuri.
Washitakiwa
wote walirudishwa rumande kwa kuwa mashitaka yanayowakabili hayana
dhamana. Mbali na mashitaka hayo, Choma anakabiliwa na kesi nyingine
yenye mashitaka 199 ya kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 15.6
katika mahakama hiyo.
Home
News
Slider
Aliyeibia Serikali Milioni 7 Kwa Dakika na mwenzake wasomewa Mashitaka Mapya 222 Kisutu.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment