Image
Image

Utata mkataba wa Machinga Complex utafutiwe ufumbuzi.

SERIKALI imebaini madudu katika mkataba wa mradi wa Jengo la Machinga Complex, ambao unahusisha Halmashauri ya Jiji la Dare s Salaam na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Utata na madudu yaliyomo katika mkataba huo vilibainishwa na ripoti ya kamati iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, baada ya kuagizwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene, Aprili 19, mwaka huu kusimamia uendeshaji wa mradi wa Machinga Complex.
Makonda, aliviambia vyombo vya habari juzi kuwa mkataba wa jengo hilo lililopo Ilala, umejaa madudu ikiwamo kutofahamika kwa thamani halisi ya ujenzi.
Mbali na utata wa gharama za ujenzi, Makonda alisema kamati yake pia ilibaini kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam halina uwezo wa kulipa deni hilo kwani jengo hilo lilipokabidhiwa kwa Jiji hilo lilikuwa na deni la Sh. bilioni 19.7, lakini hadi Machi mwaka huu, deni hilo lemefikia Sh. bilioni 38 kutoka kwenye mkopo wa Sh. bilioni 12.7.
Lingine lilikobainika katika mkataba huo, ni kutojengwa kwa ukubwa uliotakiwa wa ghorofa sita, hivyo ghorofa nne zilizopo kulifanya jengo hilo kuwa na vizimba 4,200 badala ya 10,000.
Kwamba alifanya tathmini ya haki na wajibu wa pande mbili Jiji na NSSF, na baada ya kuupitia mkataba pamoja na kukagua mradi huo, amebaini jengo hilo halikujengwa kwa ukubwa sawa na ulikubaliwa kwenye mkataba.
Aidha, fedha za mkopo ziliongezeka kutoka Sh. bilioni 12.14 kwenye mkataba na kufikia Sh. bilioni 12.7 ikiwa ni nyongeza ya Sh. milion 560 uamuzi uliofanyika bila makubaliano na kuwa, hali hiyo haimtendei haki mkopaji.
Kutokana na hali hiyo, Serikali imeimeitaka NSSF kuchukua jengo la Machinga Complex kwani deni lake la Sh. bilioni 38 halilipiki na mradi una harufu ya rushwa.
Kwa mujibu wa Makonda, mkataba huo hauna tija kwa pande zote kwa kuwa jiji halina uwezo wa kulipa deni sambamba na kufanya malipo yanayotakiwa na hauna faida vilevile kwa Machinga kwani gharama ya kupanga ni kubwa.
Ripoti inapendekeza pia kuwa licha ya NSSF kuchukua eneo lao, kwa makubalino, Halmashauri ya Jiji ilipwe kodi ya ardhi jambo ambalo linaweza kufanyika kwa urahisi kupitia NSSF na Jiji kumiliki hisa kwa pamoja.
Pamoja na kamati kutoa mapendekezo kadhaa, lakini tunazishauri pande zote zilizoko katika mkataba kukaa pamoja na kutumia busara ili kufikia maelewano na ikiwezekana kuandika upya mkataba ili kila upande unufaike.
Tunatoa ushauri huo ili lengo la kuanzishwa kwa mradi huo liendelee na walengwa wanufaike. Lengo la kuanzishwa kwa mradi huo lilikuwa kuwawezesha wafanyabiashara waliokuwa wakizagaa kwenye masoko yasiyo rasmi hasa maeneo ya Kariakoo na katikati ya Jiji la Dar es Salaam kupata nafasi za kufanyia biashara.
Baada ya kuzinduliwa kwa Jengo hilo mwaka 2010, Serikali iliahidi kuwa mradi huo ungekuwa endelevu kwa kujenga majengo mengine katika maeneo kadhaa ya Dar es Salaam kwa lengo hilo. Tunaiunga mkono hatua hiyo kwa kuwa itawapa fursa wafanyabiashara hao kufanya shughuli zao maeneo tulivu.
Tunakubaliana na mapendekezo ya kamati ya uchunguzi ya kuwachukulia hatua wahusika wote wa pande zote mbili haiwezekani kutumia fedha za mifuko za hifadhi ya jamii ambazo ni fedha za wanyonge wa taifa kwa faida ya wachache waliotanguliza ubinafsi katika utekelezaji wa mradi huo.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment