Image
Image

Watumishi saba washushwa vyeo na wengine kufukuzwa kazi.

BARAZA la Madiwani la Manispaa ya Kinondoni limewachukulia hatua za kinidhamu watumishi saba kwa kuwashusha vyeo na wengine kufukuzwa kazini, baada ya makosa waliyokuwa wakituhumiwa kuthibitika.
Miongoni mwa watumishi waliochukuliwa hatua ni Mhandisi Mkuu wa Manispaa hiyo, Hassan Mkuya ambaye ameshushwa cheo na sasa anakuwa mhandisi wa kawaida pamoja na mwenzake, Ismail Mafita aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Barabara wa Manispaa.
Meya wa Manispaa hiyo, Boniface Jacob (Chadema) alisema hayo jana wakati akisoma taarifa ya baraza la madiwani ambalo ndilo lilipendekeza kuchukuliwa hatua hizo.
“Desemba mwaka jana, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda alitoa tuhuma dhidi ya watumishi wa manispaa hasa idara ya uhandisi, baadaye mkurugenzi naye alichukua hatua ya kuwasimamisha kazi watumishi 18 waliotuhumiwa na kuwafungulia mashauri ya  nidhamu.
    “Kati ya hao 18, tisa walikuwa wa idara ya uhandisi, wanane idara ya afya na mmoja idara ya fedha. Mhandisi mkuu alikuwa akituhumiwa kwa makosa sita likiwamo la kutokufanya usanifu uliozingatia weledi hali iliyosababisha  gharama za miradi kuzidi na kushindwa kutembelea eneo la miradi na wakandarasi kusababisha hasara za barabara ya Biafra, Journalism phase 2 na ile ya Maandazi,” alisema.
Alisema tuhuma nyingine ni kutotoa cheti cha kukamilisha kazi.  Hatujui miradi kama imeshajengwa, kushindwa kusimamia miradi kwa kiwango cha kuridhisha, mfereji wa Basihaya kuwekwa  karavati zisizokuwa na kiwango na kuongezeka gharama za miradi ya barabara bila kuzingatia taratibu za  sheria za ununuzi wa umma.
“Kati ya tuhuma hizo zipo ambazo alikutwa na hatia moja kwa moja na nyingine hakukutwa na hatia hivyo ameadhibiwa kulingana na yale aliyokutwa na hatia moja kwa moja kama mfereji wa Basihaya na barabara zilizojengwa chini ya kiwango,” alisema.
Alisisitiza adhabu hizo zimetolewa baada ya uchunguzi wa kina kufanyika kwa kushirikiana na vyombo vya dola.
Uchunguzi ulifanyika kwa kwenda maeneo husika ya miradi na watuhumiwa walipewa siku 14 za kujitetea.
Alisema hata hivyo adhabu hiyo   haizuii watumishi hao kuchukuliwa hatua zaidi ikiwamo kufikishwa mahakamani.
Pamoja na hayo, daktari mmoja wa Hosptali ya Palestina, Alphonse Chiwambo amepewa onyo kali  baada ya kukutwa na kosa la kuomba rushwa ya Sh 30,000 kwa mama aliyekwenda kujifungua.
    “Lakini kuna watumishi wanne wa idara ya afya tumewafukuza kazi kwa makosa ya utoro na rushwa na watumishi sita kati ya tisa wa idara ya uhandisi wamerejeshwa kazini baada ya kukutwa hawana hatia,” alisema.
Alisema pamoja na hayo baraza liliridhia kwapandisha vyeo watumishi 372, kubadilisha vyeo watumishi tisa na kuwathibitisha watumishi 206 ambao wamemaliza vipindi vyao vya majaribio na kuonekana wanafaa kufanya kazi katika utumishi wa umma.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment