WATUMISHI
wawili wa kituo cha afya Lyabukande katika Halmashauri ya wilaya ya
Shinyanga wamesimamishwa kazi kwa uzembe uliojitokeza baada ya mjamzito
kujifungulia kwenye varanda hivi karibuni.
Akizungumza na waandishi
wa habari ofisini kwake hivi karibuni, aliyekuwa Mkurugenzi wa
Halmashauri hiyo ambaye amehamishiwa jijini Mwanza, Kiomoni Kibamba
alisema baada ya kupata taarifa hizo waliunda tume ya kwenda kuchunguza
na kubaini uzembe ndiyo ulisababisha mjamzito kujifungua kwenye varanda.
Kibamba
alisema hivi sasa wamewasimamisha kazi na kuwafungulia mashitaka ya
kimaadili ya utumishi na kuwapa siku 14 kwa utaratibu wa ajira ya
utumishi.
Aliwataja watumishi hao ambao ni Muuguzi Msaidizi, Zufa
Musa na Peter Mazengo wa kitengo cha maabara kuwa ndio walikuwa zamu
siku hiyo na kwamba walishindwa kumsaidia mzazi kitendo kilichobainika
ni cha makusudi na uzembe.
“Nilikwisha tamka siku nyingi awamu hii ya
tano ni awamu nyepesi kwa kufanya kazi sababu imenyooka na iko wazi na
mtu akienda kinyume anatakiwa kupisha ili wabaki wanaotekeleza majukumu
yao kwa mujibu wa sheria, kanuni na katiba ya nchi kwa kuwatumikia
wananchi,” alisema Kibamba.
Hata hivyo, kamati iliyoteuliwa
ikiongozwa na mganga mkuu wa wilaya, Dk Athuman Pembe ilieleza kuwa
baada ya mzazi kujifungua, watumishi hao walipata taarifa na kwenda
kumhudumia yeye na mtoto akiwa na afya nzuri mwenye uzito wa kilo tatu
na baada ya muda aliruhusiwa kurudi nyumbani.
Diwani wa Kata ya
Lyabukande, Joseph Misiri, alisema aliyejifungulia nje katika varanda la
kituo hicho ni Magreth Charles (22) aliyefika kituoni hapo akiwa
ameongozana na mama mkwe.
Inadaiwa baada ya kufika kituoni hapo saa
7:00 mchana, walielezwa hakuna huduma na siku hiyo walishauriwa waende
hospitali zingine kabla ya saa 9.30 alasiri kujifungua.
Mtendaji wa
kata ya Lyabukande, Julius Lugende alisema kuwa kituo hicho kimekuwa
kikilalamikiwa na wananchi kwa kile kinachodaiwa baadhi ya watumishi
wake hawahudumii vizuri.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment