HAPA ni kipigo tu. Hayo ni maneno ya wauguzi wa Hospitali ya Mirembe ambayo hutibu wagonjwa wa akili.
Hospitali hiyo kubwa na maarufu nchini kwa kutibu wagonjwa wenye matatizo ya akili iliyopo mkoani Dodoma, hali sasa imebadilika.
Wauguzi wa hospitali hiyo wanasema licha ya kazi ngumu inayoambatana na vipigo, wamekuwa hawapewi fedha za gharama za matibabu.
Wakizungumza
na MTANZANIA kwa sharti la kutotajwa majina yao, walisema wamekuwa
wakikabiliana na hali hiyo ikiwemo ya kupigwa na wagonjwa pindi
wanapokuwa wanawahudumia.
Watumishi waliotajwa kupata vipigo vya
wagonjwa ambao walijeruhiwa katika maeneo mbalimbali ya miili yao ni
Samwel Sumbuko ambaye alivunjwa mbavu mbili kwa kupigwa ngumi, Jackson
Marco, aliyevunjwa mkono na Sara Mwakapusya alijeruhiwa paja.
Wengine
ni Regina Kinyaiya aliyeng’atwa kidole, Stella Lutete aliyeng’atwa
pamoja na Asia Kilingo, ambaye alipigwa na kupasuliwa kichwani wakati
akimhudumia mgonjwa hospitalini hapo.
“Tunapigwa, hatulindwi,
hatusikilizwi, hatulipwi gharama za matibabu na hata tukimfuata
mkurugenzi anakujibu majibu mabaya. Na sasa imefika mahali wale wagonjwa
wakorofi tunalazimika kuwakwepa kabisa.
“Hii kazi inahitaji moyo
sana, lakini kwa kuwa ndiyo taaluma yetu tuliyosomea hatuna budi, ila
kiukweli tupo katika wakati mgumu sana, unatoka nyumbani ukiwa mzima na
ukirudi unaweza kujikuta huna meno au hata kuvunjwa mguu,” alisema mmoja
wa watumishi wa hospitali hiyo.
Kutokana na hali hiyo, alisema
wanalazimika kukwepa kuwahudumia wagonjwa wakorofi kama njia ya kunusuru
maisha yao, lakini bado uongozi umekuwa hauliangalii suala hili kwa
uzito.
“Magufuli (Rais Dk. John) si yupo kwa ajili ya wanyonge, sisi
wafanyakazi wa Mirembe tunafanya kazi katika mazingira magumu sana na
sababu ni Mkurugenzi na Katibu wake wameifanya hospitali hii ni shamba
la bibi.
“Suala la wafanyakazi kutolipwa fidia kwa muda mrefu baada
ya matukio ya kupigwa, kuumizwa na kung’atwa na wagonjwa wa akili kwetu
limekuwa ni tanuru la mateso kwani pamoja na kujaza fomu za kuomba
malipo lakini utaambuliwa majibu mabaya na kutolipwa kabisa.
“… na
haya yote yanatokana na mkurugenzi wa hospitali hii (Mirembe), ambaye
amekuwa hata akitufanya tushindwe kufanyakazi kwa moyo. Tunashindwa
kuelewa sijui tumemkosea nini Mungu—– (kilio), Magufuli njoo na hata
kwetu usikie kilio chetu nasi,” alisema mtumishi huyo huku akibubujikwa
na machozi.
Alisema pamoja na hali hiyo, Mkurugenzi wa hospitali
hiyo, Dk. Erasmus Mndeme, amekuwa akiwadhalilisha mbele ya wagonjwa na
ndugu zao bila kujali utu na hali ya mtumishi.
“Inafika mahali
wagonjwa wakati mwingine wamekuwa wakituheshimu lakini ikitokea
mkurugenzi ukamweleza suala la mgonjwa anahitaji kitu fulani utapata
majibu ambayo hutayasahau,’’ alisema.
Muuguzi mwingine alisema pamoja
na hali hiyo, wamekuwa hawalipwi stahiki zao kwa muda mrefu zikiwemo za
malipo ya utendaji wa muda wa ziada na mazingira hatari na kutokuwepo
kwa uwazi wa matumizi ya fedha za maendeleo.
Alisema muuguzi mmoja kwa siku anahudumia wagonjwa zaidi ya 100 wenye matatizo ya akili, jambo ambalo ni hatari.
“Mazingira
haya si rafiki kwani wagonjwa wa akili wengine ni wakorofi na wengine
hutaka kuwapiga hivyo kushindwa sehemu ya kukimbilia. Kuna wodi A, B na D
ambazo hutakiwa kuingia muuguzi mmoja jambo ambalo ni hatari sana,”
alisema.
Muuguzi huyo alitolea mfano tukio lililotokea Juni 19, mwaka
huu na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro
Mambosasa, mgonjwa Stella Mbalwa, alimpiga na kumuua mgonjwa mwenzake,
Halima Chedi kwa ubao kutokana na kugombea uji.
Alisema kitendo hicho ni cha hatari kwani huwafanya waishi kwa hofu huku wakihofia usalama wa maisha yao.
“Tunahudumia
hapa lakini hadi sasa unaweza kuamini kwamba hatuna hata kadi ya
matibabu ya bima ya afya kama ilivyo mahali pengine pa kazi. Hii taasisi
ipo chini ya Serikali ila haipewi kipaumbele.”
Licha ya hali hiyo
alisema kuwa wagonjwa hao wa akili kwa muda sasa wamekuwa wakipewa
vyakula na hospitali, lakini wengi wao hudhoofika kwa kukosa vyakula
vyenye vitamin inayotakiwa kwa binadamu.
Kutokana na hali hiyo
ilielezwa kuwa wagonjwa hao hutakiwa kula wali na nyama mara mbili kwa
wiki huku siku nyingine wakitakiwa kupatiwa wali na maharage na mboga za
majani.
“Inaumiza sana, ni muda mrefu wagonjwa wamekuwa wakila ugali
na maharage pamoja na uji usiokuwa na sukari mpaka mkurugenzi aamue
ndiyo wale wali. Nakwambia hivi kuna siku waligoma (wagonjwa) wakitaka
na wao wale wali na nyama, nakumbuka ilikuwa siku ya Pasaka mwaka jana,”
alisema muuguzi huyo.
MTANZANIA lilipokwenda ofisini kwa Mkurugenzi
wa hospitali hiyo, Dk. Erasmus Mndeme, ili kupata ufafanuzi wa madai
hayo aligoma kutoa ufafanuzi huku akimtaka mwandishi atoke ofisini
kwake.
“Nyie waandishi mnataka msikilizwe nyie tu sasa hivi nina
mambo yangu nayaandaa hivyo naombeni mtoke ofisini kwangu, nikimaliza
nitawapigia,” alisema Dk. Mndeme.
Kutokana na majibu hayo gazeti hili
lilimtafuta Naibu Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Dk. Hamis Kigwangalla, ili kupata maelezo ya Serikali kuhusu
madai ya wauguzi hao ambapo alisema hana taarifa za kina kuhusu madai
hayo, huku akiahidi kufuatilia ili kujua ukweli.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment