Image
Image

WAZIRI MKUU AWAFUNDA WAKURUGENZI WATEULE

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakurugenzi watendaji wateule 185 wa majiji, manispaa, miji na halmashauri za wilaya waende wakafanye kazi kwenye maeneo yao mapya waliyopangiwa kwa kuzingatia uadilifu, uwajibikaji na uaminifu.
Waziri Mkuu ametoa wito huo leo (Jumanne, Julai 12, 2016) wakati akizungumza na wateule hao kabla hawajatoa viapo ya maadili katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
“Jukumu mlilopewa na Mheshimiwa Rais ni nyeti na linahitaji utulivu na kujituma. Kila mmoja wenu anatakiwa akafanye kazi kwa uadilifu, uwajibikaji na uaminifu,” amesema Waziri Mkuu na kuongeza:
“Ninyi ndiyo injini ya maendeleo katika Halmashauri zote hapa nchini na pia mna dhamana ya kusimamia fedha za maendeleo katika halmashauri zenu. Mtajikuta mna jukumu la kusimamia fedha za ndani pamoja na fedha zinazotoka Serikali Kuu. Hakikisheni mnasimamia matumizi ya fedha hizi ili kupata value for money.”
Waziri Mkuu aliwataka wawe makini wasije wakajikuta wanaingia kwenye migogoro ya kifedha dhidi ya watendaji wengine, migogoro ya kikazi na pia migogoro na wananchi wanaoenda kuwaongoza.
“Mkifika huko ninawasihi mshirikiane na wadau wengine ambao ni wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, kamati za ulinzi na usalama, wakuu wa idara, watumishi wa idara mbalimbali zilizo chini yenu na watendaji wa kata na vijiji”, alisema.
Alisema wanatakiwa wakasome taarifa mbalimbali ili waelewe majukumu yao pamoja na mipaka yao, waelewe maeneo yao ya utawala ni yapi lakini pia wajipange kusimamia na kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwani imebeba ahadi zilizotolewa na Rais pamoja na Makamu wa Rais wakati wa kampeni za uchaguzi.
Aliwaasa pia wasiache kutafuta hotuba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kuzindua Bunge la 11, aliyoitoa Novemba 20, mwaka jana na kuwataka waisome na kufanyia kazi maeneo yote aliyoyaainisha kwa vile inatoa dira ya utendaji katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan aliwataka wateule hao watambue dhamana waliyopewa kuwa viongozi wa halmashauri na kwamba wanakwenda huko kuwa watumishi wa umma na siyo watawala.
“Wewe ni mtumishi wa watu, na watu hao pia wana wawakilishi wao ambao ni madiwani. Kwa hiyo fanyeni kazi kwa karibu na madiwani, sikilizeni shida za wananchi na pangeni vipaumbele vya kazi na pia msiache kujifunza. Soma wajibu wako kisheria na kikatiba ni upi lakini pia jipe muda wa kujifunza,” alisisitiza.
“Wewe ni kiongozi kwa hiyo tengeneza watu wako ili wakusaidie kutekeleza kile ulichotumwa kufanya. Fanyeni kazi kwa bidii kwa sababu Tanzania inaenda kwa spidi sana lakini pia mjihadhari na kashfa za matumizi mabaya ya fedha. Msisahau kuwa fedha ni fedheha, ukiitumia fedha vibaya utapata fedheha…” aliongeza.
Akiwahutubia wateule hao, Rais Dkt John Pombe Magufuli aliwataka wawe ni watatuzi wa kero za wananchi badala ya kuwa watengeneza kero na akasisitiza wawe mitume wazuri kwa wananchi.
“Kaondoeni kero kwa wananchi wa hali ya chini, wako huko wanatozwa kodi ndogondogo hata za kuuza mchicha tu. Mtu akivuna mpunga wa kula nyumbani kwake pia anatozwa kodi, ni lazima kodi hizi mkazizuie kwa sababu tuliahidi kupunguza kero kwa wananchi na siyo kuongeza kero kwao,” alisema.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment