WAZIRI
wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba jana amewasimamisha kazi
wakurugenzi watano wa idara tofauti katika wizara hiyo kutokana na
kuonesha udhaifu mbalimbali katika utendaji wao na wengine kusababisha
hasara katika usalama wa chakula.
Waliosimamishwa kazi ni Kaimu
Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Chakula nchini, Ombaeli Lemweli
kutokana na kutoa vibali vya ununuzi wa mazao na kuuzwa nje ya nchi
ilhali tathmini ikiwa haijafanyika. Nafasi yake kuchukuliwa na Elimpaa
Kiranga aliyekuwa Mkurugenzi wa Bodi ya Mazao Mchanganyiko.
Aidha,
ameagiza kusimamishwa kazi kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa
Hifadhi ya Chakula (NFRA), Charles Walwa na nafasi yake kushikwa na
Deusdedit Mpazi aliyekuwa Meneja wa NFRA kanda ya Dodoma, kutokana na
kuharibu ghala la chakula na kusababisha hasara.
Viongozi wengine wa
NFRA waliosimamishwa ni Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Huduma, Anna Ngoo,
Mkurugenzi wa Masoko, Mikalu Mapunda na Meneja wa NFRA, Songea Jeremia
Mtafya ambao wametakiwa kupisha na uchunguzi kufanyika mara moja dhidi
yao.
Kadhalika, Dk Tizeba amemsimamisha kazi aliyekuwa Kaimu
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bahari Kuu, Rashid Hoza na nafasi yake kushikwa
na Hosea Mbilinyi aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi, lengo likiwa
ni kuimarisha ulinzi wa Bahari Kuu.
Mbali na nafasi hizo, pia Mkuu wa
Kituo cha Utafiti cha Uyole mkoani Mbeya, Dk Zakaria Maly amevuliwa
madaraka na kuhamishiwa katika Kituo cha Utafiti Seliani mkoani Arusha
kuendelea na utafiti na badala yake nafasi yake itachukuliwa na Arnold
Msongi anayetoka Kituo cha Utafiti Ilonga, Kilosa mkoani Morogoro.
Dk
Tizeba alitoa maamuzi hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumzia
masuala mbalimbali, ikiwa ni mwezi mmoja baada yakuteuliwa na Rais John
Magufuli kushika wadhifa huo katika mabadiliko madogo ya Baraza la
Mawaziri yaliyompeleka aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Mwigulu Nchemba
kuongoza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri Tizeba alisema
wakati ambapo tathmini ya chakula nchini ikiwa haijakamilika, Kurugenzi
ya Usalama wa Chakula imekuwa ikitoa vibali vya chakula kusafirishwa nje
ya nchi, huku ikiwa haijulikani kama chakula kilicho kinatosha au
hakitoshi na ili ziada ilindwe.
“Mbali ya kwamba hali ya chakula
nchini ni nzuri lakini kumekuwepo na wimbi la wafanyabiashara wa ndani
na nje ya nchi wakipewa vibali na kununua mazao ndani ya nchi na kuyauza
nje ilhali tathmini ikiwa haijakamilika,” alisema Tizeba.
Alitoa
wiki mbili kuanzia sasa ukaguzi wa chakula nchini uwe umefanyika ili
kupatikana kwa tathmini halisi katika kipindi cha mwaka 2015/2016 kwani
ununuzi wa mazao hayo umeonekana mkubwa na hali hiyo isipodhibitiwa hali
itakuwa mbaya zaidi.
Alisema vibali hivyo vimekuwa vikitolewa
kinyume cha utaratibu kwa kuwa tathimini ilitakiwa kufanyika kwanza,
hivyo Katibu Mkuu amsimamishe kazi mkurugenzi huyo na uchunguzi ufanyike
dhidi yake pamoja na vibali ambavyo vimekuwa vikitolewa tangu mwaka
jana kwani havina harufu nzuri.
“Hata hivi karibuni nimepata taarifa
kuna mfanyabiashara kapewa kibali cha kusafirisha tani laki tatu
kupeleka nchini Malawi, mfanye uchunguzi wa vibali vyote alivyovitoa,”
alisema Tizeba.
Kuhusu NFRA, Dk Tizeba alisema umekuwepo udhaifu
mkubwa katika ghala la Songea, Dodoma na Sumbawanga ambako mazao
yameharibika na kusababisha hasara huku uongozi wa wakala licha ya
kuombwa vibali vya kununuliwa kwa mazao hayo kama chakula cha mifugo
havikutolewa.
Akizungumzia uvuvi bahari kuu, ameiagiza Kurugenzi wa
Uvuvi kubadilisha masharti ya leseni ya uvuvi katika bahari kuu ili
kuangalia uwezekano wa kufanya ubia na wavuvi hao ili Watanzania nao
waweze kunufaika na mavuno ya mazao hayo.
Alisema kwa wale ambao wana leseni hazitofanyiwa mabadiliko lakini kwa zile mpya na sheria haizuii kufanya hivyo.
Alisema
hivi sasa zipo meli 105 zote zikitoka nje ya nchi zikiwa zinaendelea na
uvuvi na kuchota chochote na kuondoka, huku mamlaka ya bahari wakiwa
wanayajua hayo, wakidai kuwa Tanzania haina mahali pa kushushia.
Alisema
kuanzia sasa meli zote ziambiwe mazao yote watakayovuna ambayo ni
tofauti na leseni zao zinavyotaka yaletwe Dar es Salaam, yagawiwe kama
itakavyohitajika kwani Tanzania imeendelea kuwa shamba la bibi kutokana
na kukosa uwezo wa kuvua katika bahari kuu.
Home
News
Slider
Waziri wa Kilimo Charles Tizeba ATUMBUA Wakurugenzi Watano kwa udhaifu katika utendaji kazi.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment